Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wawekezaji mazingira salama na yenye utulivu kwa miradi watakayowekeza kisiwani Pemba.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Juni 16, wakati akifungua kongamano la uwekezaji huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, likiwa na lengo la kukifungua kisiwa hicho kiuchumi.
Alisema Kisiwa cha Pemba kina utajiri mkubwa wa rasilimali, ikiwemo za bahari, hivyo amewataka wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo kisiwani humo.
Aidha, alisema maeneo huru ya Micheweni yapo tayari kwa shughuli za uwekezaji baada ya serikali kufikisha huduma muhimu za miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji), Shariff Ali Shariff, aliwataka wawekezaji na sekta binafsi kuwekeza Pemba katika miradi mbalimbali.
Alisema mazingira ya kisiwa hicho ni mazuri, na kwamba kwa sasa kazi kubwa inayofanywa na serikali ni kuimarisha mawasiliano ya bandari kwa ajili ya kuiunganisha Pemba na nchi jirani.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 1992 ilitangaza maeneo huru ya kiuchumi katika eneo la Micheweni Pemba na Fumba Unguja kwa ajili ya uwekezaji, ambapo kwa upande wa Micheweni bado uwekezaji haujashamiri. Dk. Mwinyi ameahidi katika uongozi wake wa kipindi cha pili kuimarisha maeneo hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED