TVLA yaahidi ushirikiano na wateja wake, huduma bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:51 PM Oct 09 2025
TVLA yaahidi ushirikiano na wateja  wake, huduma bora
Picha:Mpigapicha Wetu
TVLA yaahidi ushirikiano na wateja wake, huduma bora

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea kuimarisha uhusiano wake na wateja kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, yanayofanyika kitaifa kuanzia Oktoba 6 hadi 11, 2025, kwa kaulimbiu isemayo “Huduma Bora za TVLA ni Haki ya Kila Mteja.”

Akizungumza wakati wa ziara maalum katika maduka yanayouza bidhaa za TVLA jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TVLA, Furaha Kabuje, alisema lengo ni kusikiliza maoni ya wadau, wauzaji na wanufaika wa huduma za Wakala ili kuboresha huduma zinazotolewa.

Kabuje alisisitiza dhamira ya TVLA kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa, hususan chanjo za mifugo, ili kuimarisha afya ya mifugo nchini.

“Tunataka kila mteja wa TVLA apate huduma bora, salama na zenye ubora unaokidhi mahitaji ya sekta ya mifugo. Maoni ya wateja ni dira yetu ya kuboresha huduma kila siku,” alisema.

Aidha, aliahidi kuwa Wakala itaendelea kushirikiana kwa karibu na wauzaji katika maeneo ya usambazaji, elimu kwa wateja na upatikanaji wa bidhaa kwa wakati, sambamba na kuboresha mifumo ya mawasiliano kati ya TVLA na wateja wake.

Kwa upande wao, baadhi ya wauzaji wa bidhaa za TVLA waliotembelewa jijini Dar es Salaam na mkoa wa Pwani waliishukuru TVLA kwa hatua ya kuwafikia moja kwa moja na kusikiliza maoni yao. Walisema hatua hiyo inaimarisha mahusiano ya kudumu kati ya Wakala na wateja, huku wakipongeza ubora wa chanjo zinazozalishwa na TVLA.

Hata hivyo, walipendekeza kuimarishwa kwa upatikanaji wa bidhaa na mawasiliano ya moja kwa moja na ofisi za Wakala ili kurahisisha utoaji wa taarifa sahihi na huduma kwa wakati.

Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa TVLA wa kuboresha huduma, kuongeza ufanisi wa mawasiliano na kujenga mazingira rafiki kwa wateja. Kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, Wakala inaendelea kujifunza kutoka kwa wadau wake na kuimarisha maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.