CHAMA cha ACT Wazalendo, kupitia kikao cha Kamati ya Uongozi Taifa, kimelaani vikali ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa dhidi ya wananchi kuanzia Oktoba 29, mwaka huu nchini, huku kikitaka uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio hayo.
Kwa mujibiu wa taarifa iliyotolewa leo na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, ACT Wazalendo pia imesisitiza kwamba inataka wote waliohusika, waliotoa amri, waliotekeleza, au waliokaa kimya kuficha ukweli wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Pia chama hicho kimeitaka serikali ikomeshe mara moja kile kilichokiita matumizi ya nguvu dhidi ya raia na ianze safari ya majadiliano ya kitaifa kwa kusikiliza kila sauti ya wananchi.
“Madai yote ya mageuzi ya kikatiba, kisheria, kiutawala, kimfumo na kitaasisi ambayo yamekuwa yakitolewa na kupaziwa sauti tokea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi yafanyiwe kazi haraka ikiwa ni sehemu na hatua za msingi zinazohitajika kulirejesha taifa letu pamoja,” amesema Dorothy.
Ameongeza kuwa taarifa mbalimbali zimeonesha wananchi waliouawa kwa risasi, kujeruhiwa na wengine kupotea, na kwamba hadi leo wanatafutwa na familia zao.
Pia amesema chama hicho kinalaani kwa nguvu zote vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa dhidi ya wanachama na wagombea wao katika mchakato wa uchaguzi.
“Kama vile kuuawa kwa mgombea wetu wa udiwani wa kata ya Sirari Jimbo la Tarime Mkoa wa Mara Dafroza Jacob, ambaye ameuawa katika mikono ya polisi baada ya kukamatwa na kupewa mateso hadi kupelekea kifo chake Novemba 5, mwaka huu.
“ACT Wazalendo, inatoa pole za dhati kwa familia za waliopoteza wapendwa wao, na kunawaombea majeruhi wote wapone haraka. Taifa limepoteza ndugu, watoto na wazazi ambao walikuwa na ndoto za kulitumikia taifa kwa namna zao. Maumivu hayo ni yetu sote,” amesema Dorothy.
Kadhalika, alielezwa kwamba ACT Wazalendo inaunga mkono wadau na taasisi zote za ndani na nje ya nchi zilizotoa tamko la kulaani matukio hayo na kutoa mapendekezo mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED