Ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mkewe na kumfukia chooni

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:45 PM Oct 10 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi
PICHA: MARCO MADUHU
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Chimaguli Samamba (54), mkazi wa Kijiji cha Songambele Kata ya Salawe wilayani Shinyanga, kwa tuhuma za kumuua mkewe na kumfukia kwenye shimo la choo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa  tukio hilo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema kuwa mauaji hayo yaligundulika Oktoba 8 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika Kitongoji cha Ugede, Kijiji cha Songambele.

Amesema marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Moshi John (47) aligundulika kufariki dunia na mwili wake kufukiwa kwenye shimo la choo lililopo jirani na nyumbani kwake,akidaiwa kuuawa na mumewe.

“Mnamo Oktoba 1, majira ya saa 4 usiku, marehemu akiwa nyumbani kwake aligombana na mumewe ambaye alimpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili hadi kufariki dunia. Chanzo cha ugomvi huo ni mwanamke kuchelewa kurudi nyumbani,” amesema Kamanda Magomi.

Ameeleza kuwa baada ya mtuhumiwa kubaini mkewe amefariki, aliuchukua mwili wake na kuufukia kwenye shimo lililokuwa likichimbwa kwa matumizi ya choo ili kuficha ushahidi.

Magomi amesimulia  kuwa Oktoba 2 mwaka huu, majirani walianza kupata wasiwasi baada ya kutomuona marehemu kama walivyozoea, na kutokana na historia ya mumewe kumpiga mara kwa mara, walianza kupata wasiwasi na kufanya ufuatiliaji.

“Baada ya taarifa kutolewa kwa mwenyekiti wa kitongoji Oktoba 7, Polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa Oktoba 8 majira ya saa 5 asubuhi na kumkamata. baada ya mahojiano, alikiri kumuua mkewe na kumfukia kwenye shimo la choo lililopo nyumbani kwake,” amesema Kamanda.

Aidha,amesema kwa sasa Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi na haraka pindi wanapobaini matukio ya uhalifu.