Bagamoyo kuandaa mbio za vyuo vyote kutangaza utalii, kuhamasisha mazoezi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:07 PM Dec 06 2025
Bagamoyo kuandaa mbio za vyuo vyote kutangaza utalii, kuhamasisha mazoezi
Picha: Mpigapicha Wetu
Bagamoyo kuandaa mbio za vyuo vyote kutangaza utalii, kuhamasisha mazoezi

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema ofisi yake inaandaa mpango wa kufanyika kwa mbio maalum zitakazokutanisha vyuo vyote vilivyopo katika Wilaya hiyo na maeneo jirani, zikiwa na lengo la kutangaza utalii na kuhamasisha mazoezi kwa jamii.

Ndemanga ametoa kauli hiyo Desemba 6, mara baada ya kumalizika kwa mbio za Marathon zilizoandaliwa na Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM) mjini Bagamoyo.

Amesema wamekubaliana kuweka siku maalum ya mbio hizo, ambapo vyuo vya Bagamoyo vitashirikishwa kwa pamoja ili kuutangaza utalii wa wilaya hiyo, pamoja na kuimarisha afya kupitia mazoezi ya mara kwa mara.

“Ni muhimu kuwa na mijumuiko kama hii. Michezo ni sehemu ya mazoezi na njia ya kuepuka magonjwa. Taasisi zetu zimekuwa zikileta washiriki wengi kwenye michezo na hilo linapaswa kuendelezwa,” amesema Ndemanga.

Akimpongeza Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dk. Maulid Maulid, Mkuu huyo wa Wilaya amesema maandalizi ya mbio hizo yamekuwa ya mfano kutokana na mwitikio mkubwa wa washiriki kutoka ndani ya taasisi.

Awali, Dk. Maulid amesema mbio hizo zimefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu na zitakuwa endelevu, zikiwa na lengo la kutangaza ADEM pamoja na vivutio vya Bagamoyo kwa wadau mbalimbali.

Amebainisha kuwa ADEM kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya miundombinu kongwe inayohitaji ukarabati, na hivyo kupitia mbio hizo ambazo zitafanyika mara kwa mara, wadau watapata nafasi ya kujionea hali halisi na kuchangia katika maboresho.

Mtendaji Mkuu huyo aliongeza kuwa mbio hizo pia ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuandaa na kushiriki mashindano mbalimbali ya mbio katika eneo hilo.