DC Ludewa aagiza kukomeshwa uharibifu wa nyanzo vya maji Iwela

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:59 PM Oct 09 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amemuagiza Mtendaji wa Kata ya Iwela pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Iwela kuhakikisha wanakomesha uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kuwakamata na kutoza faini wote wanaoongoza mifugo yao kwenye maeneo hayo.

Thomas alitoa agizo hilo Oktoba 9, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika kata hiyo, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu uharibifu wa vyanzo vya maji unaosababishwa na mifugo.

“Hatuwezi kufumbia macho suala la uharibifu wa vyanzo vya maji ilhali tuna sheria ndogo zinazolinda rasilimali hizi. Ni lazima hatua zichukuliwe mara moja,” amesema Thomas.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza wataalamu wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani humo kuchukua hatua kali dhidi ya wananchi wanaojiunganishia maji kwa njia zisizo rasmi, akisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinaathiri upatikanaji salama wa huduma za maji kwa wananchi wengine.

Katika ziara hiyo, Thomas ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratias, pamoja na wakuu wa idara, taasisi mbalimbali na wataalamu, ambapo walifanya mikutano ya kusikiliza kero za wananchi katika vijiji vya Nsungu na Mbongo vilivyopo Kata ya Manda, pamoja na Kata ya Iwela.

Mbali na mikutano hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amekagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Nsungu–Ilela, ujenzi wa Zahanati ya Mbongo na Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwela, ambapo alisisitiza umuhimu wa kasi na ubora katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi mapema.