Dk. Mwinyi aahidi kuongeza posho za wanafunzi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:31 PM Oct 09 2025

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuongeza posho za wanafunzi wa elimu ya juu katika awamu ijayo, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na changamoto zinazowakabili katika masomo yao.

Dk. Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo wakati akizungumza na makundi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kutoka vyuo na vyuo vikuu, katika mkutano uliofanyika Chuo cha Vijana wa CCM, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema serikali yake imejipanga kuendelea kuboresha mazingira ya elimu ya juu na kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila vikwazo vya kifedha.

“Tumeona changamoto kubwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hasa katika mahitaji yao ya kila siku. Katika awamu ijayo, tutaziongeza posho ili kuendana na uhalisia wa maisha na kuwawezesha kusoma kwa utulivu,” amesema Dk. Mwinyi.

Aidha, ameahidi kuanzisha Wizara mpya ya Mawasiliano na Ubunifu katika awamu ijayo ya uongozi wake, ili kuunga mkono kazi za ubunifu zinazofanywa na vyuo na taasisi za elimu, zenye lengo la kukuza uchumi wa ubunifu na kuongeza tija kwa Taifa.

“Ubunifu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kisasa. Tunahitaji wizara mahsusi itakayosimamia sekta hii na kusaidia vijana wenye vipaji kutimiza ndoto zao,” ameongeza.

Dk. Mwinyi amewataka vijana kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza, akisisitiza kuwa vijana ni kundi lenye nguvu kubwa katika kufanya maamuzi ya kitaifa.

Ameeleza kuwa katika awamu ijayo, serikali yake itaendelea kuwapa vijana nafasi nyingi zaidi za uongozi, sambamba na kuimarisha elimu ya amali na ufundi ili kuwawezesha kujiajiri na kujitegemea.

“Tumeongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi bilioni 80 hadi bilioni 864. Lengo letu ni kuhakikisha kila kijana anaelimika na anakuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa,” amesema.

Vilevile, ameahidi kuwa serikali itaendelea kujenga vyuo vya elimu ya amali katika kila mkoa, ili kutoa fursa kwa vijana kujifunza ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.