Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa soko la Lamadi wilayani Busega, mkoani Simiyu, umechelewa kutokana na mvutano wa viongozi wa halmashauri kuhusu eneo la kujenga mradi huo, licha ya fedha tayari kutengwa.
Akizungumza leo Oktoba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Lamadi, Dk. Samia amesema ahadi hiyo aliitoa kwa wananchi wa Lamadi na kwamba serikali imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wake, lakini mvutano wa mahali pa kujenga kati ya Lamadi na Nyashimo umezuia utekelezaji huo.
“Samia Suluhu akiahidi anatekeleza. Nilitenga fedha kujenga soko, lakini uongozi wa Halmashauri unabishana lijengwe Lamadi au Nyashimo, hivyo halikujengwa. Lakini ahadi yangu iko palepale, madiwani watakapoelewana, soko lijengwe,” amesema Dk. Samia.
Amebainisha kuwa ahadi yake ya soko ni kwa ajili ya wananchi wa Lamadi, huku akifafanua kuwa Nyashimo ilipangiwa kupata stendi ya mabasi kama mradi tofauti.
“Madiwani wajue ahadi yangu ni soko Lamadi na stendi ya mabasi Nyashimo ni ahadi nyingine. Si kwamba serikali haikutekeleza, bali ni mvutano wa Halmashauri. Madiwani waelewane soko lijengwe,” amesisitiza.
Dk. Samia yupo mkoani Simiyu kwa ziara ya kampeni za uchaguzi, ambapo ameanza mikutano yake Lamadi, kabla ya kuelekea Busega na baadaye kuendelea na kampeni mkoani Mara, katika maeneo ya Bunda na Musoma Mjini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED