Uamuzi wa kesi ya Mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, kumuondoa kwenye orodha ya wagombea wa urais,umeshindwa kutolewa leo Oktoba 10,2025 kutokana na hukumu hiyo kutokamilika.
Hukumu ya shauri hilo sasa itatolewa Oktoba 15,2025 saa tatu asubuhi kwa njia ya mtandao. Akiahirisha shauri hilo, Jaji Frederick Manyanda, ambaye ndiye kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, alisema shauri hilo limekuja kwa ajili ya hukumu lakini bado hawajakamilisha kuiandaa hivyo itatolewa siku ya Jumatano Oktoba 15,2025.
Jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo linaongozwa na Jaji Frederick Manyanda, Jaji Abdallah Gonzi na Jaji Sylvester Kainda. Msingi wa shauri hilo ni hoja ya kwamba Tume Huru ya Uchaguzi ilifanya makosa ya kisheria na kikatiba, kumuengua Mpina kama mgombea urais, ikijikita kwenye mtazamo wa kisheria wa badala ya tume kufanya maamuzi ya kikatiba walizingatia ushauri na mapendekezo ya ofisi ya msajili wa Vyama vya Siasa.
Shauri hilo lilianza kusikilizwa Septemba 29, 2025, ambapo upande wa waleta maombi (Mpina na chama chake) unawakilishwa na wakili John Seka, akisaidiwa na wakili Edson Kilatu na wakili Jasper Sabuni. Katika kesi hiyo upande wa wajibu maombi alikuwa wakili mkuu wa serikali Mark Mulwambo na Erigh Rumisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED