INEC yasitisha kampeni za ubunge Siha

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 04:35 PM Oct 08 2025
INEC yasitisha kampeni za ubunge Siha.
Picha: Nipashe Digital
INEC yasitisha kampeni za ubunge Siha.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesitisha Kampeni za Uchaguzi wa kiti Ubunge katika Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, baada ya kupokea taarifa za kuuawa kwa Mgombea Ubunge wa Chama Cha Wananchi (CUF), Daud Wilbrod Ntuyehabi.

Taarifa kwa umma ya kusitisha uchaguzi wa Ubunge, Jimbo hilo, iliyotolewa na kusainiwa leo Oktoba 8,2025 na Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Siha, Marco Masue, inaeleza kuwa kutokana na kutokea kwa tukio hilo, Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Siha, umesitishwa kuanzia leo.

Sehemu ya taarifa hiyo inaeleza, “Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 71 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Namba 1 ya Mwaka 2024, na kwa barua ya tarehe 8, Oktoba 2025 isiyokuwa na kumbukumbu namba kutoka kwa Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Siha,

…Nimepokea taarifa ya kifo cha Ndugu, Daud Wilbrod Ntuyehabi, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge, Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Kutokana na kutokea kwa tukio hilo, Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Siha, Wilaya ya Siha, umesitishwa kuanzia leo tarehe 08 Oktoba 2025.”

Pia taarifa hiyo imefafanua, aidha kwa mujibu wa Kifungu cha 71 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Namba 1 ya Mwaka 2024, Tume kwa notisi itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, itapanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea na taratibu za uchaguzi wa ubunge katika jimbo husika zitaanza upya.

Hivyo, uteuzi kwa wagombea wengine ambao walioteuliwa kihalali utabaki kama ulivyokuwa awali, isipokuwa kama mgombea atajitoa na kwamba hakutakuwa na kampeni za wagombea Ubunge katika Jimbo la Siha, mpaka baada ya uteuzi wa mgombea mwingine.