Kihongosi: Vijana itunzeni amani msikubali kurubuniwa

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 08:37 PM Dec 06 2025


Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi amewataka vijana kuilinda amani na wasikubali kurubuniwa na watu wenye maslahi binafsi.

Pia, amewataka wazee kuwaelimisha watoto wao kuhusu umuhimu wa kuilinda amani, kwamba wawe mstari wa mbele katika kukemea mambo yanayoashiria uvunjifu wa amani.

Ametoa rai hiyo leo Desemba 06 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa chama na Jumuiya za CCM mkoa wa Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengineyo alisema alisilimia kubwa ya watu wanaochochea vurugu nchini wapo nje ya nchi na wanamaslahi binafsi.

"Tulinde amani, tusikubali amani yetu ivurugwe. Wazee tuwaelimishe watoto wetu, viongozi wa chama tukatimize wajibu wetu. Twendeni tukaubiri amani.
Wanaochochea vurugu wapo nje, watoto wao wanakula siagi na maziwa," amesema Kihongosi.

Kadhalika amesema CCM ni chama cha watu wote na siyo cha mtu wala watu, kwamba ni chama kinachotoa fursa kwa watu wote.

Kihongosi amesema: "Serikali inaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Kero ya kukatika kwa umeme imeanza kutatuliwa, maji yanapatikana, miradi inatekelezwa. Kwenye elimu madarasa yanajengwa"

Aliongeza: "Kwenye barabara kila eneo zinajengwa. Katika afya Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka dawa, zahanati hospitali zinajengwa. Ameagiza kutozuiwa maiti"