Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, anayeshughulikia utalii, Nkoba Mabula, amewapa 'mchongo' vijana nchini, kuwa na jicho la tatu katika fursa za uwekezaji wa masoko ya hewa ukaa (cabon) na matumizi ya teknolojia za usimamizi wa misitu kama vile ndege nyuki (drones).
Kwa sasa, Tanzania ina hekta 430,592 sawa na asilimia 31.7 ambazo zimeingia rasmi kwenye mpango wa biashara ya kaboni inayotokana na chimbuko la athari ya ongezeko la gesi joto katika uso wa dunia.
Mabula, alikuwa akizungumza leo (Desemba 5 2025) na wadau mbalimbali pamoja na wahitimu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Tazania (FITI) kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Aidha, amewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya uzalishaji wa miche ya miti, ufugaji wa nyuki wa kisasa, utengenezaji wa bidhaa za mbao zenye ubora.
"Mbali na hilo, mkawe walinzi wa rasilimali za taifa pamoja na kuwa mabalozi wema, huku mkiwa kichocheo cha shughuli za maendeleo katika jamii inayowazunguka.
“Naomba muendelee na safari yenu kwa ujasiri, nidhamu na moyo wa kujifunza kila siku. Mnavyoondoka hapa leo, mnabeba majukumu makubwa moja kulinda rasilimali za taifa, pili kuongeza thamani ya misitu, tatu kuwa mabalozi wa uchumi na mwisho kuchangia katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Mabula.
Pamoja na mambo mengine, ametoa wito kwa wakufunzi kuimarisha stadi za uongozi na maadili, akieleza kuwa katika dunia ya sasa ujuzi wa mawasiliano, uongozi na utatuzi wa migogoro ni nguzo muhimu katika jamii.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED