Mwalimu aahidi kupanua barabara Kibaha–Chalinze iwe njia nne

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 07:20 PM Oct 09 2025
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu.

Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameahidi kupanua barabara ya Kibaha hadi Chalinze kuwa ya njia nne kwa kiwango cha lami, ili kupunguza msongamano wa magari na kuongeza tija ya uzalishaji nchini.

Akizungumza katika kampeni zake mkoani Pwani, Mwalimu amesema barabara hiyo imeelemewa na magari mengi kutokana na kuwa moja ya njia kuu za kiuchumi nchini, hali inayosababisha foleni na kupoteza muda wa uzalishaji.

“Hii ndiyo barabara kubwa inayochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa taifa letu. Kupoteza muda kukaa barabarani badala ya kuzalisha kwa sababu ya foleni haikubaliki. Mkituchagua CHAUMMA, lazima tuipanue iwe njia nne kutoka Kibaha mpaka Chalinze, ili kuongeza uzalishaji na kuondoa upotevu wa muda,” amesema Mwalimu.

Ameongeza kuwa sera za CHAUMMA zinatoa kipaumbele kwa ujenzi wa miundombinu katika maeneo ya uzalishaji, hivyo barabara hiyo inapaswa kupewa umuhimu wa kipekee katika mipango ya maendeleo ya taifa.

“Hakuna sababu ya watu kupoteza muda kwa kukaa masaa mengi katika eneo dogo ambalo uwezo wa kulipatia suluhisho tunao,” amesisitiza.

Mgombea huyo wa urais wa CHAUMMA ameendelea leo na kampeni zake katika eneo la Kibaha, mkoani Pwani.