Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi wa mkoa huo kupuuza taarifa za uzushi zinazotolewa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii kuhusu vurugu wakati wa uchaguzi, na badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura. Amesisitiza kuwa Mkoa huo uko salama kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, RC Chalamila amesema Mkoa una wapiga kura zaidi ya milioni nne, na kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari imeshakamilisha miundombinu yote muhimu kwa wananchi kupigia kura. Amesisitiza wananchi wasihofu usalama wao, kwani vyombo vya ulinzi vimejipanga kuhakikisha amani imedumishwa.
Aidha, RC Chalamila amevionya vikundi vyovyote vinavyotishia kuvuruga uchaguzi kupitia mitandao ya kijamii na kubainisha kuwa vyombo vya dola viko macho kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayejaribu kuleta vurugu. Pia amewataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola iwapo wataona viashiria vya vurugu.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura bila hofu wala vurugu, akibainisha kuwa haki hiyo ni kikatiba na lazima iheshimiwa.
RC Chalamila pia amewataka vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi bila upotoshaji, kwani vyombo vya habari ni kiunganishi muhimu kati ya wananchi na Serikali. Aidha, amewataka viongozi kuanzia ngazi ya mitaa kulinda miundombinu ya Serikali, ikiwemo ya umeme na barabara za mwendokasi, na kusisitiza kuwa barabara hizo hazitumiwi na vyombo vingine vya usafiri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED