Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali atakayoiongoza itaweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za afya za mama na mtoto, akisisitiza kuwa anafahamu changamoto zinazowakabili wanawake wakati wa kujifungua.
Akizungumza leo, Oktoba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Lamadi, wilayani Busega, mkoani Simiyu, Dk. Samia amesema:
“Mimi ni mama, ninajua masuala ya kujifungua na huduma zinazohitajika, kwa hiyo nitaweka nguvu huko kwa mama na mtoto.”
Ameongeza kuwa serikali itapanua wigo wa elimu kwa kujenga shule zaidi za msingi, sekondari, na vituo vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA), ili vijana wapate ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Dk. Samia pia amegusia changamoto ya miundombinu ya maji katika baadhi ya maeneo nchini, akisema serikali itachukua hatua za haraka kurekebisha mitandao ya maji iliyochakaa na kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Aidha, ameahidi kukamilisha uunganishaji wa umeme katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na gridi ya taifa, ili kuchochea shughuli za uzalishaji, hususan katika viwanda vidogo na vya kati vinavyozalisha bidhaa zenye thamani ya juu.
“Tutahakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata umeme, kwa sababu maendeleo ya viwanda hayawezekani bila nishati ya uhakika,” amesema Dk. Samia.
Mgombea huyo wa CCM ameendelea na kampeni zake mkoani Simiyu akihimiza wananchi kuichagua CCM ili kuendeleza miradi na sera zinazolenga kuinua maisha ya Watanzania wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED