SAU-Tutajenga reli kwenye mitaa ya Mwanza kurahisisha usafiri

By Remmy Moka , Nipashe
Published at 07:58 PM Oct 09 2025

Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara.

Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara, amesema chama chake kimejipanga kuleta suluhisho la matatizo ya miundombinu nchini, hasa katika majiji makubwa, kwa kuanzisha teknolojia ya njia za reli katikati ya miji.

Akizungumza leo jijini Mwanza wakati wa mkutano wa kampeni za SAU, Kyara amesema kuwa Jiji la Mwanza litakuwa kipaumbele cha kwanza katika ujenzi wa reli mitaani kutokana na ukuaji wake wa haraka na hitaji kubwa la usafiri.

“Hatua hii inawezekana kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ulimwenguni, ambayo yamesaidia kubadilisha na kuwezesha usafiri wa uhakika pamoja na miundombinu rafiki ya usafirishaji katika majiji makubwa,” amesema Kyara.

Mgombea huyo amebainisha kuwa mradi wa reli mitaani utakuwa suluhisho la kudumu la matatizo mengi ya wananchi, kuongeza mapato ya taifa na kupunguza utegemezi kwa mataifa ya nje.

“Kwa kuanzisha teknolojia ya reli mitaani, tunalenga kuondoa changamoto za usafirishaji, kuongeza tija na kuwawezesha wananchi kujitegemea kiuchumi,” ameongeza.