Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Chunya, Mhandisi Laurent Mayala, amesema shughuli za madini wilayani humo zimeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kibiashara, huku uzalishaji wa dhahabu ukipanda kwa kasi ya kihistoria.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mayala, uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kutoka kilo 5 pekee mwaka 2017/18 hadi kufikia kilo 300 kwa mwezi kwa sasa, hali inayodhihirisha ukuaji wa sekta hiyo na mchango wake katika mapato ya Serikali.
“Mwenendo wa biashara ya madini Chunya ni wa kupongeza. Kwa mwaka 2023/24, tulizalisha dhahabu zenye uzito wa tani 3.1 zenye thamani ya Sh. bilioni 452.2, ambapo Serikali ilikusanya zaidi ya Sh. bilioni 31 kupitia tozo, mrabaha na ada za ukaguzi,” alisema.
“Kwa mwaka 2024/25, uzalishaji ulipanda hadi tani 3.9 zenye thamani ya Sh. bilioni 820.9, na Serikali ikakusanya Sh. bilioni 55,” aliongeza.
Afisa huyo alisema ongezeko la masoko na vituo vya ununuzi wa madini limechangia mafanikio hayo, ambapo kwa sasa kuna vituo vidogo 24 na soko kuu moja lililojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Chunya inatajwa kuwa mkoa wa pili wa kimadini kuanzisha soko la dhahabu nchini, ikitanguliwa na Geita.
“Hadi robo ya kwanza ya mwaka 2025/26, tumekwisha kukusanya Sh. bilioni 19.13, sawa na asilimia 26.5 ya lengo letu la Sh. bilioni 72. Tuna imani tutafikia malengo yetu,” alisema Mayala.
Kihistoria, mwaka 2023/24 Chunya ilikusanya Sh. bilioni 37.3 (asilimia 84.7) ya lengo, na mwaka 2024/25 zilikusanywa Sh. bilioni 55.37 (asilimia 92) ya lengo la Sh. bilioni 60.2.
Amesema mradi wa uzalishaji wa madini ya shaba unaoendeshwa na Kampuni ya Mineral Access Limited (MAST) umeanza kuzaa matunda, ambapo tangu kuanzishwa Aprili 2025, kiwanda hicho kilichopo Mbugani, Chunya, kimezalisha tani 810 za shaba zenye thamani ya Sh. bilioni 10.3.
Serikali imepata mapato ya Sh. milioni 594 kupitia mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Mayala alisema kiwanda cha kusafisha dhahabu kinachomilikiwa na Giant Machine’s and Equipments Ltd kimeanza majaribio na tayari kimesafisha dhahabu kilo 2.9 zilizouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na soko la nje.
Kiwanda hicho kitahudumia si tu wachimbaji wa Chunya, bali pia kutoka mikoa mingine.
Serikali, kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), ipo katika hatua za awali za kujenga maabara ya kisasa ya upimaji sampuli wilayani humo.
“Wachimbaji wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa maabara hiyo, kwani italeta ufanisi mkubwa kama ilivyo kwa Geita na Dodoma,” alisema Mayala.
Mhandisi Mayala ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza Chunya katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini, huduma za migodini na ujenzi wa mitambo ya CIP.
“Chunya bado ni hazina kubwa ya fursa. Sekta ya madini hapa ina uwezo wa kubadilisha kabisa sura ya kiuchumi ya eneo hili,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Soko la Madini Chunya, Kenneth Mwakyusa, alisema masoko yameleta unafuu mkubwa kwa wachimbaji na wanunuzi.
“Sasa hivi bei ya gramu moja ya dhahabu imepanda hadi Sh. 300,000. Serikali imetusaidia sana — Chunya ya leo si ile ya mwaka 2015,” alisema Mwakyusa.
Aliongeza kuwa masoko hayo yameongeza ajira, biashara na maendeleo, huku akitoa ombi kwa Serikali kupunguza kodi ya TRA kutoka asilimia 2 hadi 1 na kuhakikisha vifaa vya uchimbaji vinapatikana kwa bei nafuu.
Kwa sasa, Chunya inatajwa kama “Geita mpya” ya Tanzania — kitovu kipya cha dhahabu kinachofufua matumaini ya wachimbaji, wawekezaji na jamii nzima ya mkoa huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED