TLS na watetezi haki za binadamu watoa tamko

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:29 PM Nov 06 2025
TLS na watetezi haki za   binadamu watoa tamko
Picha: Mtandao
TLS na watetezi haki za binadamu watoa tamko

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wametoa tamko wakionesha kushtushwa na kuhuzunishwa na matukio makubwa ya ukiukwaji haki za binadamu yaliyojitokeza wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29.

Taarifa iliyotolewa jana kwa umma na kutiwa saini na Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa THRDC, na Wakili Boniface Mwabukusi, Rais wa TLS, imeeleza kwa kina jinsi vitendo vya ukatili na hata maafa vilivyojitokeza vinaashiria kuharibika kwa heshima ya haki za binadamu nchini.  

"Tumeshuhudia vijana wengi wakipigwa risasi, wengine kupoteza maisha na wengine kubaki na majeraha makubwa bila matibabu," wanasema katika tamko lao.  

Watetezi hao wanasema, tukio hili lingeingizwa ndani ya mjadala wa kitaifa, kwa kuwa TLS na THRDC pamoja na mashirika mengine yalijitahidi kuunda mwafaka wa amani kabla ya uchaguzi, lakini juhudi hizo hazikupokewa na mamlaka husika.  

"Tunalaani vikali mauaji na ukatili dhidi ya raia wasio na hatia. Tunataka vyombo vya usalama, hasa Jeshi la Polisi, kuheshimu haki ya wananchi kuandamana kwa amani na kuhakikisha maandamano hayageuki kuwa vurugu au kuharibu mali. Kuandamana kwa amani ni haki ya kikatiba," wanasema.  

Wamesema baadhi ya mawakili na waandishi wa habari walikumbwa na matukio makali wakiwa kazini au nyumbani. 

"Ni muhimu wazazi wapate miili ya watoto wao walioumia au kufariki ili waweze kuwazika kwa heshima," wanasema katika tamko lao.  

Vilevile, watetezi hao wanasisitiza kwamba hawauungi mkono uharibifu wa mali za umma au binafsi uliotokea wakati wa vurugu hizo. 

"Mali zote za serikali ni mali za wananchi, hivyo ni muhimu kulinda mali hizi na kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa amani, bila kuharibu mali," walisema.  

Hata hivyo, walisema uharibifu wa mali hauwezi kuwa sababu ya kutumia silaha za moto dhidi ya raia. 

"Hakuna sababu halali ya kutumia risasi za moto dhidi ya wananchi, na kuwapiga au kuwafuatilia wakiwa nyumbani mwao, huku wakiwa hawahusiki na vurugu," walisema.  

Watetezi hao wa haki za binadamu pia wameelezea kushutishwa kwa hatua ya serikali na vyombo vya usalama kuzuia upatikanaji mtandao wa intaneti, jambo lililosababisha athari kubwa kwa biashara, huduma za kibenki, huduma za afya, usafiri wa umma na binafsi, na upatikanaji taarifa muhimu kwa umma. Wamesema hatua hiyo ni kinyume cha Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za binadamu.  

Wanapendekeza hatua za haraka kurejesha utulivu, demokrasia ya kweli, uwazi na kulinda haki za binadamu ili kujenga taifa lenye amani, mshikamano na upendo.  

Hadi sasa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaendelea kulinda maeneo nyeti nchini, yakiwamo majengo ya serikali, huku baadhi ya askari wake wakionekana kuongoza magari katika makutano ya Mwenge wilayani Kinondoni na maeneo ya karibu na Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam. 

KAULI YA SERIKALI

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa Jumatatu Novemba 3, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alilaani vikali uvunjifu wa amani uliojitokeza, huku akikiri kutokea vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

"Tumesikitishwa na kuhuzunishwa na uvunjifu wa amani upotevu wa maisha, uharibifu wa mali za umma na binafsi, kwenye baadhi ya maeneo nchini hususani katika majiji na miji mikubwa.

"Kilichotokea hakiendani na Watanzania haishangazi kati ya waliokamatwa wametoka nje ya nchi. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendela na uchunguzi na kurudisha nchi katika hali ya usalama," alisema Rais Samia.

Aliagiza kamati zote za ulinzi na usalama katika mikoa na wilaya kuhakikisha hali ya utulivu inarejea mara moja, akisisitiza kuwa "machafuko hayana bei, bali mazungumzo hujenga mshikamano."

Hata hivyo, katika hotuba yake hiyo, Mkuu wa Nchi hakutaja idadi ya vifo na majeruhi. Pia hakutaja hasara halisi iliyotokana na vurugu hizo.

Juzi Jeshi la Polisi lilitoa taarifa rasmi ya kuondoa zuio la wananchi kuwa majumbani kuanzia saa 12 jioni, hatua iliyokuwa sehemu ya mikakati ya kudhibiti vurugu zilizoibuka Oktoba 29.

Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Msemaji wa Jeshi hilo, DCP David Misime, ilieleza kuwa uamuzi huo unatekeleza agizo la Rais Samia la kurejesha hali ya kawaida na kuruhusu shughuli zote za kijamii na kiuchumi kuendelea bila vikwazo.