Uhaba huduma ya maji kuwakumba wakazi Dar, Pwani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:27 PM Dec 06 2025
news
Picha Mtandao
Maji yakitoka bombani kuingia kwenye ndoo.

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewataka wananchi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kuhifadhi maji yanayopatikana na kuyatumia katika matumizi muhimu kutokana na uwepo wa changamoto ya kushuka kwa kiwango cha uzalishaji kitakachosababisha huduma hiyo kupungua.

Imesema kiwango cha uzalishaji kimeshuka zaidi ya kawaida kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa kina cha Mto Ruvu iliyosababishwa na kuchelewa kwa mvua.

Kwa mujibu wa taarifa ya dawasa iliyotolewa leo, wananchi watakao kumbwa na kadhia hiyo ni wanaohudumiwa na mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Chini kuanzia maeneo ya Bagamoyo, Tegeta, Boko, Mbezi Beach, Mwenge, Kinondoni, Mwananyamala, Masaki hadi Ilala.

“Jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ikiwemo kusitisha matumizi ya maji ya Mto Ruvu kwenye shughuli za kilimo na kuyaelekeza katika matumizi ya binadamu tu na kuongeza matumizi ya visima ili kupunguza changamoto ya ki-huduma,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mtambo wa Ruvu Juu katika maeneo ya kuanzia Kibaha, Kibamba, Kimara, Tabata, Kinyerezi, Pugu hadi Kisarawe hali ya uzalishaji maji inaendelea vizuri na huduma inawafikia wananchi.

“DAWASA inaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

1