MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema mpaka sasa imeshatoa vibali 72 vya kuruhusu wamiliki wa mabasi kuongeza mabasi ya muda ya kusafirisha abiria katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Akizungumza kwenye kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Magufuli, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, amesema katika kituo hicho cha Magufuli vibali vilivyotolewa mpaka sasa ni 31 na 41 ni katika maeneo mengine ya nchi.
Amesema wamefanya hivyo kutokana na idadi kubwa ya abiria wanaosafiri katika kipindi hiki kwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Kadhalika, akiwa kituoni hapo alfajiri baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kufanya ukaguzi na kuangalia hali ya usafiri, Suluo amesema amebaini kuwapo kwa udanganyifu kwa baadhi ya mawakala wa mabasi ambao baadhi yao walikamatwa na Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Amesema udanganyifu ambao amebaini ni kuwapo kwa baadhi ya mawakala hao ambao wanawatoza abiria nauli zaidi ya ile iliyowekwa na Mamlaka hiyo.
Pia, amesema baadhi ya mawakala walibainika kutengeneza tiketi feki za karatasi ambazo nyingine wamezitoa kopi na kuwauzia abiria wakiwaandikia magari ambayo mengine hayapo.
"Wengine tumewakamata wana tiketi za karatasi 20 mpaka 30 wameshika mkononi, kwa hiyo wanawadaka abiria na kuwauzia hizo tena kwa gharama kubwa na wanapofika kwenye gari husika huko nako wanapewa tiketi halali nyingine na wengine hizo tiketi walizouziwa hata magari hayapo kabisa.
"Kwa hiyo wengine ambao tuliwabaini kwa wakati huo tumewakamata, na tunataka sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za udanganyifu kama hizo," amesema Suluo.
Pia, Suluo amesema wamebaini baadhi ya magari kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na LATRA.
"Hili nalo ni kosa kwa sababu utaratibu uliopo, mabasi yote yanatakiwa kutumia wahudumu waliosajiliwa kwa sababu hawa wanakuwa watafahamu taratibu zote wanazotakiwa kufanya ikiwamo kuhakikisha usalama wa abiria, usafi na hata nidhamu," amesema Suluo.
Suluo amesema Mamlaka hiyo inaendelea ukaguzi na kwamba itaendelea kuchukua hatua kwa wale wote wanaokiuka sheria na taratibu za usafirishaji.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED