Viongozi watakiwa kukumbatia vipaji badala ya kuwatishia wenye uwezo

By Allan Isack , Nipashe
Published at 03:42 PM Dec 06 2025
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Laetitia Petro Ntangazwa.
Picha:Mtandao
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Laetitia Petro Ntangazwa.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Laetitia Petro Ntangazwa, amewataka viongozi wa taasisi za serikali na binafsi kuacha tabia ya kuwaondoa au kuwanyima fursa watumishi wenye uwezo mkubwa kwa sababu ya kuhofu kuonekana bora kuliko wao.

Akizungumza jana jijini Arusha katika mkutano maalum wa anuai za kitaaluma—mkutano unaowakutanisha wataalamu kutoka sekta za sheria, fedha, teknolojia na wanazuoni kwa lengo la kuwajengea uwezo—Ntangazwa alisema baadhi ya viongozi wamekuwa kikwazo kwa watumishi wenye vipaji na weledi mkubwa.

“Tuna changamoto kwenye taasisi za serikali na binafsi. Mtu ni bosi au kiongozi mkubwa, lakini anapokuta msaidizi wake ana akili na uwezo kuliko yeye, huanza kutafuta sababu za kumuondoa, kumfukuza au kumzuia kupanda cheo kwa kuhofia atachukua nafasi yake,” alisema.

Akaongeza kuwa viongozi wa aina hiyo huwanyima watumishi fursa ya kutumia karama zao kwa kuogopa kuonekana bora kuliko wakubwa wao, hali inayodumaza maendeleo ya taasisi.

“Ukiwa na watu wenye karama hizo, usiwaogope. Unapaswa kuwakumbatia, maana ndicho kinachokujenga na kukuza uwezo wa taasisi. Ukiwakandamiza, taasisi haiwezi kusonga mbele,” alisema Makamu wa Rais huyo wa TLS.

Akirejea majadiliano ya mkutano huo, Ntangazwa alisema moja ya mada kuu ilihusu uongozi jumuishi katika taasisi. Alibainisha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Mawakili, TLS ina wajibu wa kutetea haki za wananchi, ikiwamo kuhimiza utawala wa kisheria na kuendeleza uongozi jumuishi nchini.

Alisisitiza kuwa lengo la kuwakutanisha wataalamu kutoka nyanja mbalimbali ni kujenga umoja, ushirikiano, uwajibikaji, maadili ya taaluma, pamoja na kuelewa tamaduni za maeneo wanayofanyia kazi.

Kwa upande wake, Omar Mjenga—mtoa mada katika mkutano huo—alisema amewaelekeza washiriki kuhusu umuhimu wa uongozi wa kimkakati na jumuishi katika mafanikio ya taasisi.

“Bila uongozi mzuri, wa kimkakati na jumuishi, hakuna taasisi inayoweza kusonga mbele. Roho ya mafanikio ya kila taasisi duniani ni uongozi. Ukiona taasisi au serikali imeanguka, sababu kubwa ni kushindwa kwa uongozi kutekeleza majukumu yake,” alisema.

Mjenga, ambaye ni Mwanadiplomasia Mwandamizi na mbobezi katika masuala ya Itifaki, Utawala Bora na Usalama wa Kimkakati, alisema changamoto kubwa katika taasisi nyingi ni kuwatenga wafanyakazi wanaoibuka na uwezo mkubwa kielimu na kitaaluma kwa kuogopwa kama tishio.

“Watu wa aina hiyo hawapaswi kutengwa. Badala ya kuwaona kama hatari, viongozi wanapaswa kuwatumia ili kuleta mafanikio makubwa katika taasisi. Hilo ndilo niliwahimiza viongozi wa TLS waliohudhuria mkutano huu,” alisisitiza.