Wabunge wateule waitwa Dodoma, Bunge la 13 kuanza kazi Novemba 11

By Rehema Matowo , Nipashe
Published at 01:54 PM Nov 05 2025
Bunge la Tanzania
PICHA: MTANDAO
Bunge la Tanzania

WABUNGE wateule wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametakiwa kufika Dodoma kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2025 kwa ajili ya usajili na taratibu nyingine za kiutawala, kabla ya kuanza rasmi kwa vikao vya Bunge jipya Novemba 11, 2025.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, usajili utafanyika katika Ofisi za Bunge, ambapo wabunge watafanyiwa zoezi la upigaji picha na uhakiki wa nyaraka mbalimbali.Kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge la 13 kitahusisha kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika pamoja na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge wateule wametakiwa kufika wakiwa wamevaa mavazi rasmi na kuwasilisha nyaraka muhimu ikiwemo kitambulisho cha taifa na nakala yake, hati ya kuchaguliwa pamoja na kadi ya benki yenye namba ya akaunti.Nyaraka nyingine ni vyeti vya elimu au taaluma vilivyothibitishwa, cheti cha ndoa kwa walioo au walioolewa, vyeti vya kuzaliwa vya watoto walio chini ya miaka 21 pamoja na wasifu binafsi (CV).

Bunge jipya linatarajiwa kuanza kutekeleza majukumu yake ya kutunga sheria, kusimamia serikali na kuwakilisha wananchi baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais ,Waunge na madiwani uliofanyika Oktoba 29,2025. Macho na masikio ya Watanzania saa yanaelekezwa Dodoma kuona namna wabunge wapya watakavyotekeleza majukumu yao kwa manufaa ya taifa.