Wagonjwa 350 watibiwa nyonga, magoti miaka miwili Mloganzila

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:11 PM Dec 06 2025
Upasuaji ukiendelea
Picha: MNH-Mloganzila
Upasuaji ukiendelea

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, imewafanyia upasuaji wagonjwa 350 wenye changamoto ya nyonga na magoti, kwa kipindi cha miaka miwili, huku wengi wao wakiwa ni watu wazima.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MNH, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko, amesema kuna mabadiliko kwenye huduma za kibingwa, kwa kuwa mwaka 2022 walihudumiwa wagonjwa sita, hadi sasa zaidi ya 300 wamehudumiwa kwa miaka miwili.

Dk. Godlove, amasema hayo leo, Desemba 6, 2025, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi ya siku tano ya matibabu hayo, iliyoanza Desemba Mosi hadi 5, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MNH, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko
Amesema huduma hiyo imefanikiwa kwa ushirikiano na Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa na Ajali wa Hospitali ya Queen Elizabeth, Kings Lynn ya Uingereza, Prof. Mamoun Abdel Gadir, na timu yake kutoka hospitali hiyo.

Dk. Godlove, anasema uwekezaji katika sekta ya afya, ikiwamo ununuzi ya vifaatiba, kusomesha wataalam kumechangia, kuanzishwa huduma mpya ambazo zitawafanya watu wa ndani na nje ya nchi, kupata huduma na kukuza utalii tiba.

Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa na Ajali wa Hospitali ya Queen Elizabeth, Kings Lynn ya Uingereza, Prof. Mamoun Abdel Gadir
Ameongeza kuwa kutokana na ongezeko la wagonjwa wenye changamoto ya nyonga na magoti hospitali hiyo inaona wagonjwa wa kliniki wastani wa 100-150 kwa siku, na hivi sasa idara hiyo ina uwezo wa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 10-15 kwa siku.

“Kuanzia Januari hadi Desemba 2022, tulifanya upasuaji aina hii sita tu, kutokana na uchache wa wataalamu, vifaa tiba. Baada ya hapo wataalamu wamenufaika na mafunzo, kwa siku sita tu tuliweza kufanya upasuaji kwa watu 40,” amesema.

Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa aliyobobea katika Upasuaji wa Nyonga na Magoti hospitali hiyo, Dk. Shilekirwa Makira, amesema huduma za upasuaji wa nyonga na magoti nchini, umejengewa uwezo na timu ya wataalamu kutoka nchini Uingereza.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji MNH, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko (kushoto),Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa aliyobobea katika Upasuaji wa Nyonga na Magoti hospitali hiyo, Dk. Shilekirwa Makira (kulia) na Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa na Ajali wa Hospitali ya Queen Elizabeth, Kings Lynn ya Uingereza, Prof. Mamoun Abdel Gadir
Anasema manufaa ya wataalamu wa ndani kubobe kwenye tiba, kunapunguza mzigo kwa serikali katika gharama za kutibu, huku huduma hiyo iwapo ingefanyika nje ya nchi ingekuwa ni mara mbili ya fedha ambazo zinalipiwa kutibiwa nchini.

“Matibabu haya ya nyonga na magoti bandia, huwa zina muda wake. Tunatarajia baada ya upasuaji ukae kwa muda wa miaka 20-25, baada ya hapo unatakiwa kufanyika upasuaji wa marejeo. Ndio maana huwa tunawafanyia watu wazima.

“Kuna wachache ambao wanafanyiwa kwa umri mdogo wa miaka 40, maana yake akifikia miaka 60-70 atahitaji marejeo, ili kubadilisha,” anasema Dk. Shilekirwa.