Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Hussein Omary, amewasihi wahitimu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala mtambuko ikiwamo kupinga vitendo vya rushwa na ukatili wa kijinsia. Aidha, amewataka kuhakikisha wanatoa elimu jumuishi, kusimamia lishe kwa wanafunzi shuleni, na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na maambukizi mapya ya VVU.
Omary ametoa wito huo Desemba 5 mjini Bagamoyo, wakati akihutubia mahafali ya 33 ya ADEM yaliyowahusisha wahitimu 785 wa Astashahada na Stashahada.
Amesema endapo masuala hayo hayatachukuliwa kwa uzito, yanaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya elimu na maendeleo ya taifa.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado tunakabiliwa na changamoto kama utoro, ukatili, mimba za utotoni, matumizi mabaya ya madaraka, udanganyifu katika mitihani, na baadhi ya viongozi kukosa uwajibikaji. Changamoto hizi ndizo tunategemea ninyi wahitimu mzisaidie kupunguza,” amesema.
Omary amebainisha kuwa wizara yake inatarajia wahitimu hao kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuleta mabadiliko chanya katika maeneo mbalimbali ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dk. Maulid Maulid, ameziomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa elimu kuelekeza mafunzo ya maboresho ya sekta hiyo katika taasisi yao ili ADEM iweze kutekeleza kikamilifu dhima ya uanzishwaji wake. Ameomba pia mafunzo kwa sekta binafsi—ikiwamo wamiliki wa shule, mameneja na wakuu wa shule—yaendelee kutolewa kupitia ADEM.
Dk. Maulid amesema taasisi hiyo inaendelea kuhitaji fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Kampasi ya Mbeya, ikiwamo majengo ya madarasa, jengo la utawala, uzio, kantini pamoja na miundombinu mingine ya msingi. Aidha, ametaja kuwa Kampasi ya Mwanza kwa sasa inatumia majengo ya kukodi, hivyo kuiomba Wizara ya Elimu kusaidia upatikanaji wa fedha za ujenzi ili kuwezesha kampasi hiyo kuwa na majengo yake.
Amesisitiza pia umuhimu wa wahitimu kuendelea kutoa elimu kuhusu athari za uvunjifu wa amani, mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa uzalendo, akiwataka kuwafikia walimu na wanafunzi katika maeneo yao ili kuimarisha uelewa kuhusu thamani ya maadili na amani.
Katika risala yao, baadhi ya wahitimu walieleza changamoto ya kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wanapotaka kujiendeleza kielimu, ambapo Naibu Katibu Mkuu ameahidi kuwa wizara yake itashirikiana na TAMISEMI kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED