Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ametoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kikundi kidogo cha watu wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza chokochoko na maneno ya kuchochea, akisema hawawezi kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini.
Wasira ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni za urais uliofanyika Bunda, mkoani Mara, ambapo mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, alizungumza na wananchi.
Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa maneno na provokeshoni katika mitandao ya kijamii, Watanzania wengi wanathamini amani na wataendelea kuihifadhi, huku akisisitiza kuwa wachache wasioridhika hawatapata nafasi ya kutikisa umoja wa Taifa.
“Ziko chokochoko nyingi ambazo hazimo kwa watu wengi, ziko kwa wachache wanaotumia mitandao ya kijamii. Kuna watu hawaridhiki. Kama maharage yanapopikwa, lazima yapatikane machache yanayoelea juu – hayo hayaivi, na ndiyo watu wanaosumbua,” amesema Wasira.
Akimtaka Dk. Samia kutobabaishwa na maneno ya wachache hao, Wasira amesema wananchi wengi wanatambua kazi kubwa aliyoifanya Rais huyo katika kipindi chake cha uongozi.
“Hata ukifanya vizuri namna gani, kuna watakaonuna. Lakini wako wengi watakaokukumbuka kwa wema, wenye nia njema. Kama mnavyomuunga mkono hapa Bunda, ndivyo anavyoungwa mkono Tanzania nzima,” amesema.
Amesema CCM imewaletea Watanzania mgombea urais mwenye rekodi kubwa ya mafanikio, anayetekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi iliyopita, na si mtu asiye na uzoefu.
“Hatuwaletei mgombea urais ‘lena’, tunawaletea mgombea aliyefanya kazi ya urais kwa mafanikio makubwa,” amesisitiza Wasira.
Aidha, ameongeza kuwa Dk. Samia aliongoza Taifa katika kipindi kigumu kilichoshuhudia mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19, kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, na changamoto za kiuchumi duniani, lakini aliweza kuliongoza Taifa kwa utulivu na ujasiri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED