Zitto afunga kampeni kwa kishindo, akiahidi makubwa umma wafurika

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:39 PM Oct 28 2025
Zitto afunga kampeni kwa kishindo, akiahidi makubwa umma wafurika
Picha:Mpigapicha Wetu
Zitto afunga kampeni kwa kishindo, akiahidi makubwa umma wafurika

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amehitimisha kampeni zake leo Oktoba 28, 2025, kwa kuahidi kutetea maslahi na haki za wananchi wa Kigoma endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa chama hicho, Zitto amesema kipaumbele chake kitakuwa ni kuhakikisha barabara zote zenye vumbi na makorongo katika kata mbalimbali za mji huo zinajengwa kwa kiwango cha lami.

Ameeleza kuwa kipindi ambacho walikuwa wakiiongoza Manispaa ya Kigoma-Ujiji, walitengeneza mpango kabambe wa maendeleo wa miaka 20 ijayo, hivyo endapo atapata ridhaa ya wananchi, kazi ya kuendeleza mji huo itakuwa rahisi.

“Tutajenga mji ambao hauna makorongo. Tutajenga barabara zinazopitika. Mambo hayo nitayakomesha. Naomba mnipe kura za ndiyo nikasaidie watu wa Kigoma kama nilivyokuwa nikifanya kwa miaka mingi,” amesema Zitto.

Akizungumzia sekta ya afya, Zitto amesema ameshuhudia wananchi wengi wakiwa na changamoto za kiafya kutokana na umasikini, akiahidi kuanzisha mfuko wa hifadhi ya jamii utakaowezesha kila mkazi kupata huduma za matibabu kulingana na uhitaji wake.

“Ninaomba mnipe nafasi nikaangaike na afya zenu, kuhakikisha kila mtu anapata bima ya afya kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii nitakaoanzisha,” amesema huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Ameongeza kuwa atahakikisha hakuna mwanamke atalazimika kulipa fedha yoyote anapokwenda kujifungua, akisisitiza kwamba jambo hilo linawezekana endapo kutakuwepo na dhamira ya kweli ya kisera.

Vilevile, Zitto amerejea ahadi yake ya kutoa Shilingi bilioni moja kwa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali, ili kuwaepusha na mikopo yenye masharti magumu.

Kuhusu sekta ya elimu, amesema atapigania ongezeko la shule za sekondari hasa za kidato cha tano na sita, ili kuongeza fursa za elimu kwa vijana wa Kigoma.

“Ndoto yangu ni kuifanya Kigoma kuwa kituo cha biashara kikuu. Tulianza kwa kujenga bandari ya Ujiji kwa sababu mji huu uko kimkakati kwenye jiografia ya nchi za Maziwa Makuu,” amesema Zitto.

Amefafanua kuwa ana ndoto ya kuona wafanyabiashara kutoka nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi wakinunua bidhaa Kigoma badala ya kwenda Kariakoo, jambo ambalo amesema linawezekana kupitia mradi wa Ujiji City.

Zitto pia ameahidi kuendelea kutetea haki za wananchi, ikiwemo kuhakikisha raia wote wanapatiwa vitambulisho vya Taifa (NIDA) bila ubaguzi.