LEO ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula Duniani. Huadhimishwa kuongeza wigo wa uelewa kuhusu ugonjwa huo. Fistula huwakumba wanawake katika umri wowote, kwa wasichana na watoto wa kike ambao walizaliwa na tatizo.
Bingwa wa Magonjwa ya Kinamama na Mfumo wa Uzazi kutoka hospitali ya CCBRT, Dk. Peter Majinge, amefanya mazungumzo maalum mwandishi wa Nipashe Digital, kuadhimisha siku hiyo, akiyataja mafanikio yaliyofikiwa na hospitali hiyo wakishirikiana na wadau.
Bingwa huyo ana angalizo la ujio kuwapo kwa fistula inayokua kwa kasi, itokanayo na kasoro wakati wa upasuaji, hasa kwa wanaojifungua kwa njia ya operesheni ‘ceaser’, njia ya mkojo inapoguswa na kupata jeraha ama marija wa mkojo kutoka kwenye figo, huwa chanzo cha ugonjwa.
“Kuna ongezeko la fistula iliyotokana na kasoro za upasuaji wakati wa ‘ceaser’ mfumo wa mkojo ukipata jeraha, kwa bahati mbaya, itasababisha mama huyo kuvuja mkojo bila kujitambua, hiyo fistula tayari,” anasema.
Kadhalika, Dk. Majinge anazitaja changamoto zilizopo kwa wanaougua ugonjwa huo, unyanyapaa kutoka kwenye jamii inayowazunguka na ndugu wa familia wa karibu hata wenza kuwatenga wenzao.
“Kwanza jamii inauona ugonjwa huu ni aibu kutokana na ulivyo. Haja ndogo humtoka muda wowote kwa anayeugua, bila yeye kujijua, atajitenga, hachangamani na jamii, akitaka kutoka ajistiri sana,” anasema bingwa huyo.
Dk. Majinge ambaye pia ni Bingwa wa Upasuaji wa Fistula, amefafanua ugonjwa huo, tangu alipoanza kufanya tiba zake, akiwa ni tatibu aliyedumu kwa zaidi ya miaka 10 kazini hadi sasa. Haya ndiyo mahojiano kati yake na mwandishi.
Swali: Fistula ni nini, kwa lugha rahisi ili kila mtu aelewe.
Jibu: Kuna fiistula aina tofauti kutokana na sababu ya chanzo cha ugonjwa huo. Fistula ya uzazi ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokea kati ya njia ya uzazi na kibofu cha mkojo. Pia tundu hilo linaweza kutokea kati ya njia ya uzazi na haja kubwa.
Itasababisha mtu kutokwa haja kubwa ama ndogo bila kujizuia. Sababu kubwa hasa fistula ya uzazi, ni uzazi pingamizi, ambao hufanya kichwa cha mtoto kukwama katika nyonga za mama, wakati anajifungua na ikiwa kwa muda mrefu tundu linaweza kutokea katika haja kubwa au ndogo.
Swali: Je, tatizo likoje kwa hapa nchini? Takwimu za wanaougua.
Jibu: Tunatumia takwimu ambazo zinaandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kwa kila mwaka kwetu Tanzania kinamama 3,000 wanapata changamoto hii ya fistula.
Linasema kwa upande wa huduma ni kinamama wasiozidi 1,500 wanaweza wakapata huduma zinakotolewa huduma. Wengi hawajafikiwa. Ingawa kuna wadau wengine wanatoa huduma, kwa ujumla ukijumlisha wote watoa huduma tunawafikia kinamama 1,500 kwa mwaka.
Swali: Tiba ya ugonjwa huu ikoje, ni lazima mgonjwa kufanyiwa upasuaji?
Jibu: Kwa ujumla matibabu ya fistula, hufanyika kwa njia ya upasuaji. Ingawa kuna kinamama ambao tunaweza kuwagundua mapema sana baada ya kupata changamoto hiyo wakawa na matundu, tunawaacha na mrija wa mkojo wa takribani wiki mbili au tatu. Tundu linaweza kuziba upasuaji wowote. Ila wengi huwa lazima uwafanyie upasuaji
Tukishamfanyia mama upasuaji wa fistula anakaa na mpira wa kutolea haja ndogo wiki mbili, kisha baada ya hapo hupimwa kama tundu limezibwa.
Swali: Awali ulisema wanaougua ugonjwa huu, hukumbwa na unyanyapaa kwenye jamii, ni kwa namna gani?
Jibu: Kubwa ni kwamba, kinamama wengi waliopatwa na fistula, jamii inawatenga. Kwa sababu ya changamoto wanazopitia, wengi wanatokwa na haja ndogo au kubwa, bila wao kujizuia, hivyo wanatoa harufu ya hizo haja, na watu wengi wanawaweka mbali na jamii.
Mfano kwenda sokoni, kanisani, msikitini hawaendi. Tunawafundisha hizo stadi, kufuma, kushona inawasaidia kuwa wazalishaji, kupata kipato.
Na kwa bahati mbaya zaidi waume zao wanakuwa wamewaacha na mbaya zaidi hii fistula huwapata walio na umri madogo. Lengo ni kuwaunganisha tena na jamii.
Swali: Ni sababu nyinge ya fistula mbali na hii fistula itokanayo na uzazi?
Jibu: Kuna sababu nyingine zinajumuishwa na fistula. Kuna kinamama pia ambao wanapata fistula sababu ya upasuaji, kwa bahati mbaya kama mama amepata jeraha kwenye kibofu cha mkojo, wakati wa kumtoa mtoto tumboni baada ya upasuaji.
Pia, fistula inaweza kutokana na upasuaji wakati wa kutoka uvimbe. Kwa bahati mbaya daktari anaweza akagusa na kukata kibofu ama akakata mrija unaotoa mkojo kutoka katika figo kuleta kwenye kibofu unaitwa ‘urethra’.
Sababu nyingine ni saratani. Mama anaweza akapata saratani ya kibofu cha mkojo au shingo ya uzazi, ikizidi sana inaweza kuleta changamoto ya fistula.
Sababu inayofuata pia ni ajali, nyonga yake ikajeruhiwa na kusababisha hata kibofu cha mkojo kujeruhiwa.
Swali: Fistula kwa watoto wadogo husababishwa na nini na hasa katika umri gani?
Jibu: Kuna watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa na fistula, huyu ni mtoto ambaye anatokwa na mkojo muda wote, utakuta hata shuleni kule anachekwa au anajikojolea, anapewa adhabu kumbe alizaliwa na kasoro.
Wanaokuja na tatizo la fistula hasa kwa kujifungua yaani uzazi wa utotoni ni wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18.
Pia, kuna zaidi ya changamoto ya fistula. Wapo akinamama hupata tatizo wakati wakijifungua kwa njia ya kawaida na wakachanika msamba. Huyu hana tofauti sana na aliyepata fistula kwa njia ya haja kubwa, atashindwa kuzuia haja. Wengi wanafikiri kwamba mama akishajifungua maumbile hubadilika huwa hivyo, lakini hiyo si hali ya kawaida ni tatizo ambalo linaweza kutibika.
Wengi tunawagundua wakija kwenye uchunguzi wa kawaida, tunaona sehemu zake haziko kawaida, tunawatengeneza na kurejea kwenye hali ya kawaida. Tunawafanyia upasuaji. Baada ya kuchanika msamba kuna ushonaji hufanyika wa aina mbili.
Kwanza kwenye chumba cha kujifungukia ‘labor’ hapo hapo. Lakini baadhi ushonaji baada ya pale unakuwa sio toshelevu na kusababisha misuli ya kubana haja kubwa haibani, anashindwa kujizuia. Mwingine alishonwa vizuri tu lakini anapata zile-gaping’ (uwazi), labda sababu ni maambukizi, kasoro ushonaji hewa inapita. Wakija tunawarudia tena.
Swali: Kwa nini huduma hii inatolewa bure, kwa sababu gharama zake ni kubwa na mwananchi wa kawaida asingemudu kama ilivyo kwa magonjwa sugu kama vile Kifua Kikuu (TB)?
Jibu: Tulitafuta wadhamini, kuja na mradi. Kutoa matibabu kwa wenye fistula, kwa sababu kama nilivyosema hapo awali wengi huwa wametengwa na jamii, wanashindwa kujitokeza, tunaona mama anayeugua anazungukwa na vizuizi vingi.
Kuna mama alikuja akiwa na fistula iliyodumu kwa miaka 60. Alianza kuugua akiwa na miaka takribani 23 na alikuja hapa na kuanza matibabu akiwa na miaka 83. Sababu ni kujifungua.
Alikaa na hiyo changamoto kwa muda mrefu wapo ambao hukaa na changamoto hiyo kwa muda mrefu. Tulipofanya utafiti tukabaini hakuna uelewa, gharama, imani potofu kwenye jamii.
Wengine huenda hadi kwa waganga wa kienyeji. Tukaangalia namna ya kusaidia jamii ili kutaua changamoto hiyo, wengi wao wako huko vijijini. Tumewaweka mabalozi ndani kabisa huko vijijini kwa kuwatambua, kuwaleta kwenye huduma, tunatumia nauli na kuwarudisha.
Vijijini ni wengi zaidi kutokana na miundombinu ni changamoto, licha ya kwamba hivi sasa serikali imeboresha huduma za afya zimetanuka. Tumeona kupungua kidogo kwa fistula za uzazi.
Swali: Fistula inatibika kabisa?
Jibu: Kuna kinamama wachache lakini tunasema fistula hii haitibiki ambao sehemu kubwa ya kibofu imejeruhiwa, lakini huwa tunafanya upasuaji mkubwa zaidi kwa kuwageuzia njia. Pamoja na kwamba lile tundu halijazibwa, tunaunganisha haja ndogo kupitia haja kubwa kwa pamoja.
Baada ya upasuaji kuna masharti ya kuishi nayo kwa siku 90 wasishiriki tendo la ndoa. Tunawashauri kinamama hivyo, ili kuzuia jeraha lisisumbuliwe hadi lipone.
Tunawafuatilia baada ya kutoka hapa, kwanza ufuatiliaji miezi mitatu, sita, mwaka, kule walipo wanatumika mabalozi kutupa mrejesho au tunawasiliana na eneo la huduma inapofanyika.
Swali: Kwa kasi gani unaona upasuaji ule kweli ulikupa simulizi isiyosahaulika?
Jibu: Kuna upasuaji unafanyika ambao unaona umerejesha tabasamu kwa mama, nafarijika sana. Changamoto kuna ambao wanakuja mrija umekatwa kabisa, hata ukimfanyia upasuaji na anatoka bado analoa, yeye anaona bado hajapona, lakini unamwelewesha kwamba hiyo ni tiba ya kwanza utarudi tena.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED