Yanga kwenda mahakamani ni kuhujumu CHAN, AFCON

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:43 AM May 12 2025
Yanga kwenda mahakamani  ni kuhujumu CHAN, AFCON
Picha:Mtandao
Yanga kwenda mahakamani ni kuhujumu CHAN, AFCON

SOKA la Tanzania halipo salama. Kama kwenye kilichosemwa na baadhi ya wanachama na wazee wa Yanga kuwa moja ya maazimio yao ni kwenda mahakamani kudai haki yao, basi nadhani Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), linaweza kuzuia fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN), kuchezwa hapa nchini.

Kwa bahati mbaya sana michuano hiyo pia itachezwa kwenye nchini za Kenya na Uganda, hivyo ni rahisi zaidi kuziondoa timu au kundi lililopangwa kuchezwa mechi zake hapa na kupelekwa huko.

Labda tu wanaotaka kufungua kesi wachelewe kwenda huko, lakini ikiwahi hali inaweza kuwa mbaya, kwani michuano hiyo inatarajiwa kupigwa, Agosti 2 hadi 30, mwaka huu.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam, wanachama hao wa Yanga, pamoja na mambo mengine, waliahidi kuwa watakwenda mahakamani ili kuzuia kutangazwa bingwa wa Tanzania Bara, lakini pia wanataka liitwe Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), na Bodi ya Ligi ili lielezee mkasa mzima na sababu ya kuahirishwa kwa dabi, iliyokuwa ichezwe, Machi 8, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Labda kama ni propaganda, au wameongea hivyo ili kushinikiza kile ambacho wanakisimamia, lakini kama ni kweli, si tu wanaliweka soka la Tanzania pabaya, lakini hata klabu yenyewe ya Yanga inaweza kufungiwa kwa kupeleka suala hilo mahakamani.

Nadhani hata viongozi wa Yanga wanajua ubaya au madhara ya kufanya kitu hicho, ndiyo maana hawajatoa  au kuichapisha habari hiyo ya wanachana na wazee wa klabu hiyo kwenye peji zao za mitandao ya kijamii, ikiwamo, instagram.

Wanachama hao wakae wakijua kuwa kitendo cha kwenda mahakamani kuzuia bingwa kutangazwa hiyo moja kwa moja ni kuingilia soka linalochezwa na matokeo yake kupatikana uwanjani pamoja na kanuni zake na kuingilia waliopewa dhamana ya kuuongoza mpira wenyewe.

Ndiyo maana FIFA ikasisitiza kuwa mambo ya soka hayapelekwi mahakamani. Mechi inachezwa leo inaisha maisha yanaendelea, haiwezekani itokee timu iende kupinga mahakamani kwani itabidi isubiri hata miezi sita ili uamuzi wa mechi moja tu utolewe. Je, hiyo ligi itakuwa inaisubiri mahakama iamue?

Nadhani wanachama wa Yanga wangeheshimu maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (CAS), ambayo ndiyo imewekwa na FIFA kushughulikia masuala hayo.

Kwa bahati nzuri Yanga ilitumia vizuri uhuru wao kwa kupeleka shauri lao huko, lakini iligonga mwamba. Hicho ndicho chombo cha mwisho, hivyo hakuna namna nyingine.

Kujaribu kutafuta haki kwenye vyombo ambavyo vimepigwa marufuku na FIFA, ni kama kutaka kujikaanga kwenye mafuta.

2007, Tanzania pia itakuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika, kama jambo hili litaendelea kunaweza kutuweka kwenye hatari pia na kupokonywa.

Ni kwa sababu FIFA watakapoifungia Tanzania mpaka hapo tutakapomaliza matatizo yetu ya ndani, kila kitu kitakuwa kimevurugika.

Kingine ambacho wanachama na Yanga hawakitambui, ni kwamba kama TFF na Bodi ya Ligi wataelekeza kilichojiri na kuamua kupeleka mahakamani, klabu inaweza kufungiwa, ama kucheza Ligi ya Ndani au mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Klabu inaweza kufungiwa kwa sababu waliopeleka kesi mahakamani ni wanachama na si viongozi.

Kama watapeleka viongozi basi FIFA watadili na viongozi hao na si klabu, lakini kwa hii naona wanachama ndiyo wanataka kuitia shimoni timu yao.

Tusifikie huko, nadhani ifike wakati viongozi wa Yanga wakae na wanachama wao na kuwaambia madhara ya kwenda mahakamani kwa klabu yao na taifa kwa ujumla, vinginevyo hata wao wanaweza huko mbele kulaumiwa na hao hao wanaotaka kupeleka kesi huko.