Muunganisho wa intaneti umerejeshwa nchini Uganda saa chache baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliomalizika hivi punde.
Siku ya Jumanne (Januari 13), Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) ilitangaza kuwa inasitisha huduma za mtandao kufuatia "pendekezo" kutoka kwa kamati ya kitaifa ya usalama.
UCC ilichukuwa hatua hiyo ili kuzuia usambazaji wa taarifa ghushi, wizi wa kura, pamoja na shinikizo la mtandaoni linaloweza kuchochea ghasia au vurugu.
Shirika la kutete haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilielezea hatua hiyo kama "kusumbua sana"
Hata hivyo, hatua za kuminya upatikanaji wa intaneti wakati wa chaguzi si jambo geni nchini Uganda.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, huduma za intaneti zilikatizwa kwa takribani wiki moja, hatua ambayo iliwaathiri zaidi ya watumiaji milioni 10 wa huduma hiyo.
Kurejeshwa kwa huduma za mtandao kunaweza kutafsiriwa kama ishara ya imani ndani ya vikosi vya usalama kwamba nchi imeepuka hali ya wasiwasi iliyoenea wakati wa uchaguzi, sawa na ilivyoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita.
Hata hivyo,ghasia zinazohusiana na uchaguzi zimeripotiwa katika maeneo tofauti ya nchi, kama vile Mukono na Bwaise viungani mwa jiji la Kampala.
Ripoti zinadai makabiliano yalizuka kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani.
Muda mfupi baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa Alhamisi kwa asilimia 72, mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye alipata asilimia 25, alitoa taarifa kwa njia ya video kupinga matokeo hayo akiyataja kuwa ''feki''.
Ametoa wito kwa wafuasi wake kupinga matokeo hayo kwa kujitokeza na kuandamana kwa amani dhidi ya kile alichosema ni juhudi za kuhujumu mchakato wa kidemokrasia.
Chanzo: BBC
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED