WHO yalaani Marekani kujiondoa rasmi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:22 PM Jan 25 2026
WHO yalaani Marekani kujiondoa rasmi
Picha: Mtandao
WHO yalaani Marekani kujiondoa rasmi

‎Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza masikitiko yake kufuatia uamuzi wa Marekani kujiondoa rasmi katika shirika hilo, likisema hatua hiyo inaongeza hatari kwa Marekani na usalama wa afya duniani kwa ujumla.

‎Marekani ilitoa notisi ya kujiondoa Januari 20, 2025 kupitia amri ya Rais Donald Trump, na kujitoa rasmi Januari 22, 2026, ikieleza nia ya kufanya kazi za afya moja kwa moja na mataifa mengine bila kupitia mashirika ya kimataifa.

‎WHO imesema taarifa ya kujiondoa itajadiliwa katika kikao cha Bodi ya Utendaji Februari 2, 2026 na Mkutano wa Afya Duniani Mei 2026. Shirika hilo limekanusha madai ya Marekani kuwa limeharibu heshima na uhuru wake, likisisitiza kuwa limekuwa likishirikiana na Marekani kwa nia njema na kwa kuheshimu mamlaka yake ya kitaifa.

‎Kuhusu lawama za Marekani juu ya mwitikio wa WHO katika janga la UVIKO-19, shirika hilo limesema lilitoa mapendekezo ya kiafya kama matumizi ya barakoa, chanjo na umbali wa kimwili bila kulazimisha sera hizo, na liliarifu dunia mapema kuhusu hatari ya ugonjwa huo tangu taarifa za awali kutoka China mwishoni mwa mwaka 2019.

‎WHO pia imeeleza kuwa ni shirika huru na lisiloegemea upande wowote, linaloongozwa na nchi wanachama 194, na limeendelea kuimarisha mifumo ya maandalizi na mwitikio dhidi ya majanga. Aidha, limepongeza nchi wanachama kwa kupitisha Mkataba wa Janga la WHO unaolenga kuimarisha usalama wa afya duniani.

‎Kwa sasa, WHO inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa kushirikiana na nchi zote, huku ikieleza matumaini kuwa Marekani, kama mwanachama mwanzilishi aliyetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya afya ya umma duniani, itarejea kushiriki kikamilifu katika shirika hilo siku zijazo.