‘Magonjwa NCDs bado mzigo’

By Rahma Suleiman , Nipashe Jumapili
Published at 03:48 PM Jan 25 2026
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa Wizara hiyo, Dk. Marijani Msafiri Marajini
Picha: Rahma Suleiman
Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa Wizara hiyo, Dk. Marijani Msafiri Marajini

Wizara ya Afya Zanzibar, imesema serikali inatumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza, yakiwamo shinikizo la damu, kisukari na saratani.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba wa Wizara hiyo, Dk. Marijani Msafiri Marajini, amesema kutokana na kasi ya ongezeko la wagonjwa wa maradhi hayo, wizara kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imeandaa kambi maalum ya uchunguzi wa afya bure kwa wananchi wa Zanzibar.

Amesema kambi hiyo ya huduma za kibingwa na kibobezi katika uchunguzi wa maradhi yasiyoambukiza itafanyika kwa muda wa siku nne kuanzia Februari 3 hadi 6, mwaka huu, katika viwanja vya New Amani Complex.

Dk. Marajini amesema mwenendo wa maradhi umebadilika ikilinganishwa na miaka ya nyuma, magonjwa ya kuambukiza kama UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria yalikuwa yakiongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani.

Amefafanua kuwa kwa sasa maradhi yasiyoambukiza ndiyo chanzo kikuu cha vifo duniani, yakiongozwa na magonjwa ya moyo, yakifuatiwa na saratani na kiharusi, yanayotokana na shinikizo la damu na kisukari.

Dk. Robert Moshiro kutoka MNH, amesema kambi za uchunguzi na matibabu ni endelevu, ambapo tangu kuanza kwake mwaka 2023 zaidi ya wananchi 3,500 wameshanufaika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Amesema kwa Zanzibar wanatarajia kuwafikia wananchi zaidi ya 5,000 huku akibainisha kuwa katika kambi zilizofanyika awali, magonjwa yaliyogundulika kwa wingi ni shinikizo la damu, maradhi ya ngozi, kisukari pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.

Ameongeza kuwa kambi hiyo itahusisha watoa huduma 30 kutoka MNH na 10 kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, madaktari bingwa 14 pamoja na wauguzi wabobezi watakaoshirikiana kutoa huduma hizo.