Ubovu barabara, uhaba umeme vyakwamisha elimu Busongo

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 03:17 PM Jan 25 2026
Mkurugenzi wa shule hiyo, David Moses
Picha: Marco Maduhu
Mkurugenzi wa shule hiyo, David Moses

Ubovu wa miundombinu ya barabara na ukosefu wa huduma ya umeme katika eneo la Busongo, Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, umetajwa kuwa kikwazo cha maendeleo ya kijamii katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa shule ya Awali na Msingi ya Hope Conscious, David Moses, amesema hayo na kuwa kukosekana kwa huduma hizo, vinawaathiri wananchi wa eneo hilo.

Amesema hasa gharama ni katika sekta ya elimu, kutokana na kutumia gharama kubwa kuchapisha mitihani, huku vyombo vya usafiri vikiharibika mara kwa mara.

“Eneo hili la Busongo tunakabiliwa na changamoto kubwa ya ubovu wa miundombinu ya barabara na ukosefu wa umeme, tunaiomba serikali ichukue hatua za haraka kututatulia,” amesema Moses.

Wanafunzi wa shuleni hapo
Amesema, shule hiyo licha ya kusajiliwa mwaka jana,  kwa sasa wapo hatua ya darasa la tano na wanajumla ya wanafunzi 82, wasichana 52 na wavulana 30.

Amesema kuwa,  mbali na elimu ya darasani, shule hiyo pia imejipanga kuanzisha shughuli za ziada zikiwamo ufugaji wa mifugo, bustani, utengenezaji wa sabuni na viatu, pamoja na kuanzisha maabara ya utafiti na ubunifu, ili kukuza stadi na vipaji vya watoto.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Shinyanga Salome Komba, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Alixius Kagunze, amesema changamoto hizo amezibeba na watakwenda kuzifanyia kazi, ili zipate ufumbuzi.

Aidha, amewataka wazazi na walezi, kuwapeleka watoto kuandikishwa shule ambao tayari wameshafikia umri wa kuanza masomo, ili kuwapatia haki yao ya kielimu na kutimiza ndoto zao.