Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga Ustaadhi Rajabu Abdallah amesema ana dhamira ya dhati kurejesha timu ya mpira wa miguu, African Spots ya jijini humo, ili kurejesha heshima ya timu hiyo kongwe.
Amesema timu hiyo imekuwa ikisuasua kupanda daraja kwa muda mrefu sasa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwamo basi la kuwasafirisha wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Ustaadhi Abdallah ameyasema hayo jana katika hafla ya kuukabidhi uongozi wa timu hiyo gari lipya aina ya TATA lililogarimu takribani Sh. milioni 170, iliyofanyika nje ya Ofisi zao zilizopo barabara ya 12 jijini hapa.
"Kurudi kwa timu hii kongwe ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1936, kutarejesha heshima ya Mkoa wa Tanga kwani bila African Spots hakuna Coastal Union, timu hizi mbili ni watani wa jadi halisi kuliko hata Simba na Yanga," amesema.
Mbali ya kununua basi na kukabidhi, mwenyekiti ameahidi kuboresha timu hiyo na kuiinua hadi kufikia kucheza ligi kuu.
Sambamba na kukabidhi gari hilo mwenyekiti huyo pia alitoa kiasi cha Sh. milioni 30 na kukabidhi kwa uongozi wa timu ya Coastal Union, kwa ajili ya kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili.
Rais wa TFF nchini Walles Karia, amewasihi wanachama kushirikiana na vionhozi ili kufanya maamuzi pamoja na kujitokeza uwanjani pindi timu zitakapokuwq zancheza kwani ndio jambo sahihi la kuvuta wawekezaji.
Lakini pia amewasihi viwanja vya michezo vilivyopo Myanjani Technically Center, "kile kituo kipo na kinafanya vizuri sana lakini kinanufaisha vijana walioko nje ya Tanga, niwasiji kwamba mpeleke vijana pale ili timu zetu zipate wachezaji bora," amesema Karia.
Katika hafla hiyo alikuwapo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) ambaye amesisitiza suala la wanachama kushirikiana na viongozi wa timu hiyo na kuchangia kipato kwenye timu matokeo yataonekana.
"Kama tutakuwa na timu mbili (2) zinazoenda ligi kuu, hata uchumi wa Tanga utaimarika kupitia michezo, tuchangie timu kwa kwenda uwanjani na hata kununua jezi, kwa kufanya hivyo kutaimarisha timu zetu na wachezaji kuwa na ari uwanjani," amesema.
Naibu Waziri Mwana FA, ametoa kiasi cha Sh. milioni 10, kila timu imekabidhiwa kwa vionhozi wa timu zote mbili kiasi cha Sh. milioni tano.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dk. Batilda Buriani amewataka viongozi wa timu za mipira na wanamichezo wote kutumia fursa ambazo zipo mkoani humo katika kuimarisha timu na kuleta manufaa katika mkoa.
"Mradi wa Bomba la mafuta nao una fursa katika michezo, kule Uganda wamesaidia kujenga uwanja wa mpira na hata timu yetu ya Coastal Union, imeshapeleka maombi yake tunasubiri utekelezaji mwengine uendelee," amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED