Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amezindua jengo jipya la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chalinze, huku akiwapongeza kwa kuonyesha uzalendo wa kuokoa Sh. milioni nane katika fedha za ujenzi zilizotengwa na kutumika Sh. milioni 406.4 kati ya 414.6 zilizotengwa.
Amesema kilichofanywa na taasisi hiyo ni funzo kwa wengine huku aksisitiza kwamba, serikali itaendelea kuwa wakali kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika kama zilivyopangwa na miradi inakamilika kwa kiwango kinachotakiwa.
Vilevile amewataka watendaji wa taasisi za umma nchini kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wa maeneo husika pindi wanapotekeleza miradi ya serikali, huku akisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya wananchi katika maeneo yanapotekelezwa miradi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema mradi huo ambao umetekelezwa na ofisi ya TAKUKURU Chalinze, ulianza Mei, 2024 na ulikabidhiwa Januari, 2025 ukiwa umekamilika.


Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Domina Mkama, amesema jengo lililokuwa linatumika awali ambalo ni la kukodi, walishindwa kuweka miundombinu ya mawasiliano, huku wananchi wakishindwa kuwafikia kutokana na eneo waliko.
Mkama amesema jengo hilo jipya lina mazingira rafiki ya wananchi kutoa taarifa tofauti na la awali, ambalo wengi walikosa uhuru wa kuifikia taasisi hiyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED