DC Msando akabidhi mtambo wa kusafisha maji chumvi Mburahati

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:06 PM Jan 25 2026

‎
‎Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,  Albert Msando
Picha: Mpigapicha Wetu
‎ ‎Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,  Albert Msando

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amekabidhi mtambo wa kuchakata na kusafisha maji ya chumvi wa thamani ya zaidi ya Sh. milioni 125 kwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Mburahati, ikiwa ni hatua ya Serikali kumaliza changamoto ya muda mrefu ya maji safi na salama kwa wananchi wa kata hiyo.

‎Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Msando alisema mradi huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali, kamati ya kata na wadau wa maendeleo, akisisitiza kuwa mtambo huo ni mali ya wananchi na unapaswa kusimamiwa na kulindwa ili kupunguza kero ya maji.

‎Alieleza kuwa Kamati ya Maendeleo ya Kata ina jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo maji, afya na elimu, akibainisha kuwa maji ni msingi wa maendeleo na yana mchango mkubwa katika kulinda afya ya jamii.

‎Katika hatua nyingine, Msando alitoa onyo kwa viongozi, vikundi na watu binafsi waliopokea mikopo ya halmashauri kupitia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kushindwa kurejesha, akisema Serikali haitavumilia matumizi mabaya ya fedha za umma.

‎Kwa mujibu wake, Halmashauri ya Ubungo ina mikopo inayozunguka yenye thamani ya Sh. bilioni 14, lakini kiwango kilichorejeshwa ni kidogo, hali inayozuia wananchi wengine kupata mikopo. Aliagiza watendaji wa kata na Manispaa kuchukua hatua za kisheria kwa wadaiwa wote ili fedha zirejeshwe na kuelekezwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji.

‎Msando alihitimisha kwa kuwataka wananchi na viongozi kushirikiana kulinda miradi ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi wote.