Wananchi Itwangi walia ubovu wa barabara

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 02:47 PM Jan 18 2026
Mwananchi Kulwa Kashinje, mkazi wa Kijiji cha Butini Kata ya Itwangi wilayani Shinyanga, akionesha ubovu wa barabara ambayo imekatwa na maji
Picha: Marco Maduhu
Mwananchi Kulwa Kashinje, mkazi wa Kijiji cha Butini Kata ya Itwangi wilayani Shinyanga, akionesha ubovu wa barabara ambayo imekatwa na maji

Wananchi wa Kata ya Itwangi wilayani Shinyanga, wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kukarabati miundombinu ya barabara.

Wamedai kuwa hali imekuwa mbaya zaidi kipindi cha mvua kiasi cha kushindwa kwenda mashambani na watoto kukosa masomo kutokana na hatari ya kusombwa na maji.

Wamebainisha hayo jana, wakati wakizungumza na waandishi wa habari, walipotembelea maeneo hayo korofi ya miundombinu ya barabara, mara baada ya kuibuliwa kero hiyo, kwenye mkutano wa hadhara wa Diwani wa Itwangi Lidya Pius.

Wananchi Itwangi walia ubovu wa barabara
Wamesema barabara nyingi ndani ya kata hiyo zimekatwa na maji, hali inayosababisha shughuli za kilimo kusimama pamoja na watoto kushindwa kufika shuleni pindi mvua zinaponyesha.

Mkazi wa Kijiji cha Butini Roja Samweli, amesema barabara ya kwenda Mwakasong’we imekuwa ikikatwa mara kwa mara na maji kiasi cha wanakijiji kulazimika kuchangishana fedha kununua bomba kwa ajili ya kutengeneza karavati za kienyeji, lakini juhudi hizo hazikudumu.

“Kilio chetu ni ubovu wa barabara, tunaomba serikali itusikie. barabara zimekatwa na maji, maisha yetu yapo hatarini, mvua zinaponyesha tunashindwa kwenda mashambani na kufanya shughuli zetu za kila siku,” amesema Samweli.

Mwananchi mwingine, Grace Mihambo, ameomba serikali kuwajengea daraja katika Mto Mayaya, unaotumiwa na wakazi kuvuka kwenda mashambani pamoja na watoto wanaosoma Shule ya Msingi Welezo.

Amesema mvua zinaponyesha, mto huo hujaa maji na kuwazuia watoto kuhudhuria masomo, huku njia hiyo ikiwa ndiyo pekee inayowaunganisha na shule, pamoja na wao kwenda shambani.

Kulwa Kashinje, amesema wakati wa mavuno, wakulima hulazimika kuacha mazao mashambani kutokana na kushindwa kuyasafirisha kwa sababu ya ubovu wa barabara.

“Maji yanapoongezeka tunashindwa kupitisha mazao, na kuamua kuyaacha shambani hadi maji yapungue,” amesema Kashinje.

Awali akijibu kero hiyo kwenye mkutano wa hadhara, Diwani wa Itwangi Lidya Pius, amesema tayari ameshawasilisha changamoto ya ubovu wa barabara kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), ambao wameahidi kuzifanyia ukarabati baada ya kufika kukagua maeneo husika.

Amesema haridhishwi na hali ya miundombinu ya barabara katika kata hiyo, na ndiyo sababu ameiweka kuwa kipaumbele chake, akiahidi kuendelea kufuatilia hadi upatikane hata mfuko wa dharura, kwa ajili ya kukarabati barabara hasa zilizokatwa na maji.

Mwakilishi wa Meneja wa TARURA wilayani Shinyanga, Mhandisi Thobias Francisco, amesema barabara ya Itwangi–Mwakasong’we, imejumuishwa kwenye mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema barabara ya Nsalala–Butini imepangwa kutekelezwa mwaka wa fedha 2027/2028, sambamba na barabara ya Welezo–Mwakasong’we inayopita kwenye mto, akisisitiza kuwa barabara zote zimeshafanyiwa tathimini na zitakarabatiwa awamu kwa awamu.