Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, katika ofisi yake jijini Dodoma, Januari 29, 2026, ambapo wameonesha nia ya kuimarisha ushirikiano na kuwekeza katika Biashara ya Kaboni.
Katika mazungumzo hayo, Masauni amemshukuru Balozi Tinnes kwa kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Norway na Tanzania, huku akieleza kuwa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kinaendelea kuimarika kadri siku zinavyosonga mbele, hatua inayoongeza ufanisi katika usimamizi wa biashara hiyo.
Aidha, Waziri Masauni ameeleza mpango wa Serikali wa kutoa elimu kwa umma kuhusu Biashara ya Kaboni kuanzia ngazi za juu hadi kwa wananchi wa kawaida, lengo likiwa ni kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo muhimu.
Pia ameongeza kuwa Taifa linaendelea kujidhatiti katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama mojawapo ya mikakati ya kulinda na kuhifadhi mazingira nchini, sambamba na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED