Wanafunzi 30 wa Kitengo cha Petroleum Engineering kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) leo Januari 30, 2026 wametembelea Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa lengo la kujifunza kwa vitendo kuhusu utendaji kazi wa wakala huo pamoja na utekelezaji wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) nchini.
Ziara hiyo ilifanyika chini ya Chama cha Wahandisi wa Mafuta (Society of Petroleum Engineers – SPE), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwaunganisha wanafunzi na uhalisia wa kazi katika sekta ya mafuta.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Lojistiki za Mafuta PBPA, Mhandisi Sophia Kidimwa, amesema wanafunzi hao wamepata fursa ya kuelewa kwa kina mchakato mzima wa upatikanaji wa mafuta nchini kuanzia hatua za uagizaji hadi usimamizi wa lojistiki za kupokea mafuta.
“Tumejikita kuwaelimisha kuhusu taratibu zote za uagizaji wa mafuta, jinsi yanavyoingia nchini, mchakato wa uletaji wake pamoja na faida za Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS),” amesema Mhandisi Kidimwa.
Ameongeza kuwa PBPA imekuwa ikiendelea kupokea wageni kutoka taasisi mbalimbali wanaopenda kujifunza kuhusu mfumo wa BPS kutokana na mafanikio na manufaa yake kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mhandisi wa PBPA, Prudence Laurean, amesema wanafunzi hao walipitishwa katika mifumo yote ya PBPA, kuanzia hatua za uagizaji wa mafuta hadi yanapofika kwenye maghala ya kuhifadhia, ikiwemo matumizi ya Mfumo wa SCADA katika ufuatiliaji wa mafuta wakati wa kushushwa kutoka melini kwenda kwenye maghala ya Serikali na binafsi.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Sifrina John, mwanafunzi wa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema ziara hiyo imelenga kuunganisha nadharia na vitendo.
“Tumekuja kuunganisha yale tunayojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi, pamoja na kuelewa kwa vitendo namna PBPA inavyosimamia uagizaji na ugavi wa mafuta nchini,” amesema Sifrina.
Ameongeza kuwa wanafunzi wamefurahishwa na mafunzo waliyoyapata pamoja na mchango wa PBPA katika uchumi wa Taifa.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa juhudi za PBPA katika kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali nchini, sambamba na kukuza uelewa wa vijana kuhusu mifumo ya kimkakati inayosimamia sekta ya mafuta na maendeleo ya uchumi wa Taifa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED