Vijana wa kikundi cha YES GROUP katika Wilaya ya Karagwe, Kata ya Kayanga, Mkoa wa Kagera wamefanikiwa kujikwamua kiuchumi kwa kutengeneza mafuta, mbolea asilia na chakula cha mifugo baada ya kupata mkopo.
Mkurugenzi wa Halmashauiri ya Wilaya ya Karagwe, Happiness Msanga alisema jana kuwa kikundi hicho ni sehemu ya wanufaika wa mikopo ya vijana ambao walikopeshwa shilingi milioni 65.
Alisema walipata mkopo huo kwaajili ya shughuli aina tatu za kiuchumi ambapo shughuli ya kwanza wanazalisha mbolea za asili, kuzalisha mafuta na uzalishaji wa chakula cha wanyama.
“Halmashauri tulianza kuwawezesha kwa awamu na wameendelea kukua tangu waanze mwaka 2021 tumeona ni kikundi cha kuiga na cha mfano kwetu kwani wameweza kujitosheleza mahitaji yao na familia zao na kukuza kikundi,” alisema na kuongeza
“Hawakuanza na vyote walianza na kimoja kimoja na kadri tunavyoshirikiana nao unaona wanavyozidi kukua kwa hiyo halmashauri ya wilaya ya Karagwe tunajivunia kuwa na kikundi hiki vijana hawa wanaleta taswira kwenye jamii kuwa vijana wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi badala ya kukaa vijiweni,” alisema
Alisema kimejikita katika utengenezaji wa mbolea ya asili, shughuli inayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
“Kupitia mikopo ya maendeleo ya vijana, kikundi kiliwezeshwa na mkopo wa asilimia 10% wa shilingi 15,000,000 pamoja na mkopo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) Sh. 50,000,000,” alisema.
Ili kuwa na kilimo endelevu kwa vitendo, alisema kikundi cha YES Group hutengeneza mbolea ya asili kwa kutumia mabaki ya vyakula na malighafi rafiki kwa mazingira.
Aidha, alisema mbolea hiyo inarutubisha udongo kwa muda mrefu na husaidia kuongeza mavuno kwa wakulima kwa udongo kutunza unyevunyevu unyevu kwa muda mrefu.
Alisema mbolea hiyo inafaa kwa aina zote za mimea, ni rafiki kwa ardhi na mazingira kwa ujumla na mbali na mbolea ya asili, kikundi pia kinajihusisha na utengenezaji wa mafuta ya alizeti, uzalishaji wa vyakula vya mifugo, uongezaji wa thamani kwenye madini ya chumvi na shughuli mbalimbali za kilimo biashara.
“Miradi hiyo imekuwa chachu ya kuhamasisha vijana wengi kuondokana na mtazamo hasi kuhusu kilimo na badala yake kukiona kama fursa ya kiuchumi yenye tija,” alisema.
Alisema manufaa kwa Vijana na Jamii kupitia uwezeshaji huu, vijana wa YES Group wameweza kujiajiri na kuongeza kipato, kupata ujuzi wa vitendo katika kilimo na uzalishaji na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengine.
“Vijana wa kikundi hiki wamechangia usalama wa chakula katika jamii ambapo upatikanaji wa mbolea ya asili kwa bei nafuu umeongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima wadogo,” alisema.
“Ufanisi wa YES Group unaonyesha wazi manufaa ya mikopo ya vijana kwa halmashauri na kuongezeka kwa vyanzo vya mapato na kodi kutoka kwenye shughuli za uzalishaji,” alisema
Alisema faida nyingine kwa halmashauri ni kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana, kuimarika kwa uchumi wa ndani wa wilaya, kukuza sera za kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe inanufaika kwa kuona vijana wake wanakuwa wazalishaji, walipa kodi, na mabalozi wa maendeleo jumuishi.
“Ujumbe kwa Vijana Wengine ni kwamba YES Group ni ushahidi kuwa mikopo ya vijana ikitumika vizuri inaleta mabadiliko ya kweli,”.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED