Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, imeandikisha zaidi ya wanafunzi 8,300 wa darasa la awali kwa mwaka huu wa masomo.
Imeelezwa kuwa kuna ongezeko la mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto wao shule.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Erica Yegella ameyasema hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Amesema kwa darasa la kwanza wameandikisha wanafunzi 900 na kwa kidato cha kwanza wameandikisha wanafunzi 6523 ambao wameandikishwa katika shule mbalimbali za sekondari katika halmashauri hiyo.
Amesema kutokana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi, halmashauri hiyo imeendelea kutumia mapato ya ndani na fedha kutoka serikali kuu kuboresha miundombinu mipya ikiwemo vyumba vya madarasa, madawati na vyoo.
Amesema ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa sekondari na msingi linachochewa na vitu mbalimbali ikiwemo sera ya elimu bila malipo kwa sekondari za serikali.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED