Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imezuia utekelezaji na matumizi ya Kanuni ya 4(4)(a) na (b) ya Kanuni za Uwajibikaji wa Kijamii (CSR) kwa Wamiliki wa Leseni za Madini, ikisema kuwa kanuni hizo zinakinzana na Sheria ya Madini na zinanyonya jamii zinazozunguka migodi.
Mahakama pia imebaini kuwa Waziri wa Madini alishindwa kushirikisha jamii mwenyeji kabla ya kutunga na kuchapisha kanuni hizo zilizotangazwa Juni 23, 2023, jambo lililokiuka misingi ya kisheria na haki za jamii husika.
Uamuzi huo umetokana na maombi yaliyofunguliwa na wakazi wa vijiji vya Matongo, Nyangoto, Mjini Kati na Kewanja (North Mara) wilayani Tarime, wakipinga mgao wa asilimia 40 ya rasilimali za CSR kwa jamii mwenyeji badala ya asilimia 100 iliyokuwepo awali.
Waombaji walidai kuwa kanuni hizo zilitungwa bila wao kushirikishwa na zimepunguza kwa kiasi kikubwa manufaa yao ya kiuchumi, kijamii, kimazingira na kiutamaduni, huku Waziri wa Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakitetea kuwa kanuni hizo zilitungwa kwa mujibu wa sheria na baada ya mashauriano ya wadau.
Hata hivyo, Jaji Kamazima Kafanabo alisema Mahakama imejiridhisha kuwa waombaji wameathiriwa moja kwa moja na mgao huo mdogo, na kusisitiza kuwa Sheria ya Madini na Kanuni za CSR zinaelekeza rasilimali za CSR kunufaisha jamii mwenyeji bila kugawanywa.
Mahakama ilieleza kuwa endapo Bunge lingekuwa na nia ya kugawa rasilimali hizo kwa halmashauri, lingeweka wazi katika sheria, na kwamba kitendo cha Waziri kuanzisha mgawanyo huo kilikuwa nje ya mamlaka ya kisheria na ni hujuma ya kiutawala.
Kutokana na hoja hizo, Mahakama ilitoa amri ya kufuta uamuzi wa Waziri wa Madini wa kutunga kanuni hizo, ikitangaza kuwa Kanuni ya 4(4)(a) na (b) ni batili, haina nguvu ya kisheria na imezuiwa kutumika au kutekelezwa nchini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED