Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imekiri kuwepo kwa changamoto ya urejeshaji wa mikopo kwa baadhi ya vikundi vilivyonufaika na asilimia 10 ya mapato yasiyofungwa, hali inayokwamisha vikundi vingine kupata fursa hiyo.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dk. Maria Kapinga, amesema hadi sasa jumla ya Sh.milioni 625 zimekopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema licha ya utoaji wa mikopo hiyo, bado kuna changamoto ya baadhi ya vikundi kutorejesha kwa wakati,hivyo aliwataka warejeshe ili kuwakopesha watu wengine ili nao waweze kunufaika.
“Natumie fursa hii kuvisihi vikundi vilivyokopeshwa kurejesha mikopo yao kwa wakati aidha, vikundi vilivyokidhi masharti viendelee kuomba mikopo kupitia mfumo rasmi, huku Idara ya Maendeleo ya Jamii ikiendelea kufanya uhakiki kabla ya utoaji wa mikopo mingine,” amesema Dk. Kapinga.
Katika taarifa hiyo, amesema Manispaa ya Ilemela imekusanya zaidi ya Sh.bilioni 7 sawa na asilimia 42.9 ya makisio ya mapato ya ndani ya Sh. bilioni 16.45 kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26.
Amesema kati ya fedha zilizokusanywa, asilimia 60 zilitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu na afya.
Katika sekta ya elimu, fedha zilitumika katika ununuzi wa madawati na ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kwa upande wa sekta ya afya, fedha zilitumika kutekeleza miradi ya ujenzi wa zahanati za Nyambiti na Nyafula pamoja na kuboresha huduma za upasuaji katika Kituo cha Afya Kayenze.
Anaeleza kuwa katika kipindi hicho, Manispaa imetekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 43.9 kupitia mapato ya ndani, ruzuku kutoka serikali kuu pamoja na fedha za Mpango wa Uendelezaji Miji na Majiji (UCDG).
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED