slot gacor
slot gacor
slot gacor
Wananchi Isaka waomba ajira mradi wa reli | Nipashe

Wananchi Isaka waomba ajira mradi wa reli

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 01:03 PM Jan 30 2026
 Wananchi Isaka waomba ajira mradi wa reli
Picha: Marco Maduhu
Wananchi Isaka waomba ajira mradi wa reli

Wananchi wa Kata ya Isaka, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameomba vijana wa eneo hilo kupewa kipaumbele cha ajira wakati wa utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa reli ya kati utakaotekelezwa kuanzia Aprili 2026 hadi 2029.

Ombi hilo limetolewa jana wakati Maafisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) walipotoa elimu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo kutoka Dar es Salaam hadi Isaka. Wakizungumza kwa niaba ya wananchi, Said Hamadi alisema mradi huo ni wa kimkakati na umefungua fursa za ajira na uchumi, hivyo vijana wa Isaka wanapaswa kupewa kipaumbele.

Diwani wa Kata ya Isaka, Pazi Majuto, amesema ukarabati wa reli hiyo utaifanya Isaka kuwa kitovu muhimu cha uchumi kutokana na uwepo wa bandari kavu na faida za usafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi TRC, Aikande Munuo, alisema TRC si mwajiri wa moja kwa moja bali itamsimamia mkandarasi kuhakikisha vijana wa eneo la mradi wanapewa ajira. Alibainisha kuwa reli hiyo ina urefu wa kilomita 392.4, huku kipande cha Tabora–Isaka kikigharimu dola milioni 200 (takribani Sh bilioni 500) kwa mkopo wa Benki ya Dunia.

Munuo alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa makaravati na madaraja 171 pamoja na mabwawa sita ili kupunguza athari za mafuriko, huku ukilenga kukuza uchumi kupitia sekta ya usafirishaji, umwagiliaji na ufugaji.

Naye Afisa Usalama wa mradi, Justine Kalokola, amewataka wananchi kulinda miundombinu na kuzingatia tahadhari za usalama, wakati Mwanasheria wa TRC, Jane Kassanda, ametoa onyo kali kwa watakaohujumu reli au kutoa rushwa, akisisitiza hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.