Umoja wa Ulaya umeorodhesha Jeshi la Mapinduzi la Iran kama kundi la kigaidi, kufuatia ukandamizaji mkali wa maandamano ulioua maelfu ya watu.
Hatua hiyo, ilitangazwa leo Ijumaa na inaongeza shinikizo kwa Iran
Mkuu wa sera za kigeni wa EU, Kaja Kallas, amesema mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama walikubaliana kwa kauli moja juu ya uamuzi huo.
Amesema hatua hiyo inaliweka jeshi hilo katika daraja moja na makundi kama Al-Qaida, Hamas na IS.
"Wanaotumia ugaidi lazima watendewe kama magaidi,” amesema Kallas.
Maandamano hayo, yaliyochochewa na matatizo ya kiuchumi, yaligeuka kupinga utawala wa kidini wa Iran, kabla ya kutumia nguvu kubwa kuyamaliza.
Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, ukandamizaji huo umeua takribani watu 6,443.
Nchi nyingine kama Marekani na Canada tayari zilishalitaja Jeshi la Mapinduzi la Iran kuwa kundi la kigaidi huko nyuma.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED