Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, leo Januari 30, 2026, imekutana na Wakili Peter Madeleka jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo pia tume hiyo imekutana na taasisi mbalimbali binafsi zilizopata fursa ya kuwasilisha maoni yao kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.
Akizungumza baada ya kukutana na tume, Wakili Peter Madeleka amesema kuwa aliwasilisha maoni yake kuhusu matarajio na uhalali wa tume hiyo. Amesema alirejea kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyowahi kutoa kuhusu kilichotokea siku ya uchaguzi, akieleza kuwa Rais alisema matukio hayo hayakuwa maandamano bali yalikuwa ni jaribio la mapinduzi.
Madeleka amebainisha kuwa, kwa mujibu wa kauli hiyo, watu waliodaiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi walikamatwa, wakashtakiwa na baadaye kusamehewa, na kwa sasa wako huru uraiani. Hata hivyo, amesema kuna maswali mazito yanayohitaji majibu kuhusu watu waliouawa wakati wa matukio hayo.
Amehoji ni kwa nini mauaji yalitokea ilhali wanaodaiwa kuhusika na mapinduzi wamesamehewa na kuachiwa huru, akisisitiza kuwa waliouawa hawakuwa na hatia yoyote kwa kuwa hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya waliodaiwa kuhusika na machafuko.
Kwa mtazamo wake, Madeleka amesema lawama haziwezi kuelekezwa kwa vyama vya upinzani, bali askari waliodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani ili haki iweze kupatikana.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED