Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeagizwa kuhakikisha inafikisha huduma ya umeme katika vitongoji vyote ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa leo na Frank Mugogo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi kutoka kampuni ya Central Electricals International Ltd anayetekeleza Mradi wa HEP 2B katika vitongoji 218 mkoani Njombe.
Mugogo amesema agizo hilo limetolewa na serikali, ambapo katika Mkoa wa Njombe yenye vitongoji 1,833, kati ya hivyo 1,276 tayari vina huduma ya umeme huku vitongoji 557 vikiwa bado havijaunganishwa.
“Mradi huu utafikisha umeme katika vitongoji 218, hivyo vitongoji vitakavyobaki bila umeme vitakuwa 339 ambavyo navyo vitakamilishwa baadaye,” amesema Mugogo.
Ameongeza kuwa gharama za kuunganisha umeme ni Sh. 27,000 tu, na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Njombe kutumia fursa hiyo ya kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu iliyowezeshwa na Serikali.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Lewisi Mnyambwa, ameishukuru serikali kwa kutoa zaidi ya Sh bilioni 24 kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji vya mkoa huo.
“Serikali kupitia REA imefanya kazi kubwa, tunasisitiza miradi hii ikamilike kwa muda uliopangwa, na tutaendelea kuisimamia ipasavyo ili mkandarasi aweze kutekeleza majukumu yake bila changamoto yoyote katika kipindi chote cha utekelezaji,” amesema Mnyambwa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED