Mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 11 robo ya kwanza ya mwaka 2025 hadi asilimia 12 robo ya pili, hatua inayoonesha kuimarika kwa sekta hiyo.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde, akitoa taarifa ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mchango huo umeongezeka kwa kasi ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2020 na asilimia 10.1 mwaka 2024.
Amesema kati ya Julai na Desemba 2025, tani 14.66 za dhahabu zenye thamani ya Sh. trilioni 3.75 ziliuzwa katika viwanda vya kusafisha dhahabu nchini, huku hadi Desemba 2025 Serikali kupitia BoT ikinunua tani 17.03 zenye thamani ya Sh. trilioni 4.97, hatua iliyoimarisha akiba ya dhahabu ya Taifa.
Mavunde ameongeza kuwa Novemba 2025 hadi Januari 25, 2026, Wizara ya Madini ilikusanya Sh. bilioni 311.80 sawa na asilimia 111 ya lengo, na Julai hadi Desemba 2025 ikakusanya Sh. bilioni 653.94 sawa na asilimia 108.99 ya lengo la kipindi hicho. Mafanikio hayo yametokana na maboresho ya sheria, usimamizi wa leseni, udhibiti wa biashara ya madini na mapambano dhidi ya utoroshaji wa madini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED