Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika soko la zamani la Maganzo, wapewe kipaumbele cha kurejea katika soko jipya, baada ya kukamilika kujengwa.
Ametoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa la Maganzo.
Amesema, wafanyabiashara wa awali ambao walikuwa wakifanya biashara katika soko hili, hao ndiyo wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuingia katika soko hili jipya.
Nao baadhi ya wafanyabiashara hao akiwamo Simon Andrew, wameiomba serikali kukamilisha haraka ujenzi wa soko hilo jipya, ili waondokane kufanya biashara katika mazingira ambayo siyo rafiki.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa soko hilo Hilda Hozza kutoka Mgodi wa Mwadui, amesema linajengwa kwa gharama ya Sh. milioni 260, likiwa na vizimba 200, na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED