slot gacor
slot gacor
slot gacor
Vikundi 30 vyapewa sh. milioni 490 mkopo wa asilimia 10 Shinyanga | Nipashe

Vikundi 30 vyapewa sh. milioni 490 mkopo wa asilimia 10 Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:40 PM Jan 19 2026
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (kulia) akikabidhi mfano wa hundi sh. milioni 490.6 fedha za mikopo asilimia 10 mapato ya ndani ya halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa vikundi 30, vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (kulia) akikabidhi mfano wa hundi sh. milioni 490.6 fedha za mikopo asilimia 10 mapato ya ndani ya halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa vikundi 30, vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Jumla ya vikundi 30 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Shinyanga vimepatiwa mkopo wa jumla ya shilingi milioni 490.6, fedha zitokanazo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Kati ya fedha hizo, vikundi tisa vya vijana vimepatiwa shilingi milioni 170.6, vikundi 20 vya wanawake vimepata shilingi milioni 318, huku kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kikipewa shilingi milioni mbili.

Mkopo huo ulikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kwa mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 490.6, katika hafla iliyohusisha wanufaika wa makundi maalumu yaliyolengwa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhita alisema utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ni mkakati wa Serikali wa kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kwa kuwapatia mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

“Mikopo hii haina riba, hivyo nawasihi wanufaika wote kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe na tija na kuwainua kiuchumi,” alisema Mhita.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Shinyanga, Peres Kamugisha, alisema manispaa itaendelea kutenga fedha za mikopo ya asilimia 10 kupitia mapato ya ndani, ili kuhakikisha makundi hayo yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Manispaa ya Shinyanga imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya mikopo hiyo.

“Leo tumetoa shilingi milioni 490.6 kwa vikundi 30, ambapo vikundi tisa vya vijana vimepata shilingi milioni 170.6, vikundi 20 vya wanawake shilingi milioni 318, na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu shilingi milioni mbili,” alisema Kamugisha.

Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, akiwamo Richard John, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba, wakisema mikopo hiyo imekuwa mkombozi dhidi ya mikopo ya kausha damu inayotozwa riba kubwa na kusababisha wananchi wengi kupoteza mali zao wanaposhindwa kufanya marejesho.