Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba anatarajia kuzindua meli ya Mv. New Mwanza kesho.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa meli hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali na ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Kanda ya Ziwa.
Akizungumza leo Januari 22 na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu mradi huo , Waziri Mbarawa ameeleza kuwa meli hiyo imejengwa kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria, mizigo na magari ndani ya Ziwa Victoria.
Amesema hatua hiyo inatarajia kuongeza ufanisi wa safari na kuimarisha uchumi wa wananchi wa mikoa inayozunguka ziwa hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamissi, amesema Mv. New Mwanza itasafirisha mizigo na abiria Bukoba kupitia Kemondo, na baadaye kuelekea Uganda na Kisumu nchini Kenya.
Hamissi amesema meli hiyo ina uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo, abiria 1,200, pamoja na magari madogo 20 na makubwa matatu.
Aidha, meli hiyo imejengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 120.56, ina ghorofa nne, urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17.
Ameongeza kuwa safari za majaribio zilizoanza Machi 2025 tayari zimesafirisha abiria 7,028 na mizigo takribani tani 673, ikiwa ni ishara kuwa meli hiyo ipo tayari kuanza kutoa huduma kwa kiwango kikubwa baada ya uzinduzi wake.
Wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wameeleza matumaini makubwa kuhusu meli hiyo wakisema itapunguza usumbufu wa safari, kuongeza usalama wa abiria na mizigo, pamoja na kufungua fursa mpya za biashara.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED